Na Yohana Paul, Geita
JUMLA ya kina mama 17,616 wamejitokeza kufunga kizazi mkoani Geita ndani ya kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2017 hadi 2021 ikiwa ni njia ya kupanga uzazi waliyoichagua kwenye vituo mbalimbali vya afya.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto mkoa wa Geita, Daniel Sinda katika mahojiano maalumu na Mtanzania Digital juu ya mwelekeo na mwitikio wa matumizi ya uzazi wa mpango mkoani hapa.
Daniel amesema, takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2017 pekee takribani kina mama 6,210 walijitokeza kupata huduma ya kufunga kizazi kwa mkoa mzima ambapo mwaka mmoja baadaye (2018) idadi ilishuka hadi kina mama 4,373.
Amebainisha, kwa mwaka 2019 kina mama 2,179 walifunga uzazi na idadi ilipanda kwa mwaka 2020 na kufikia kina mama 2,928 huku kwa mwaka 2021 idadi ya kina mama waliojitokeza kufunga kizazi ilishuka hadi 1,926.
Ameeleza, mbali na kufunga uzazi, pia wengine wameendelea kujitokeza kutumia njia zingine za uzazi wa mpango ambapo kwa takwimu za mwaka 2021 pekee takribani kina mama 8,439 walisajiliwa kutumia vidonge vya uzazi wa mpango.
Aidha Daniel amefafanua, kwa mwaka huo 2021 kina mama 27,296 walijitokeza kupanga uzazi kwa njia ya sindano, kina mama 42,488 walipanga uzazi kwa njia ya vipandikizi (njiti) huku kina mama 12,151 walijitokeza kupanga uzazi kwa nji ya kitanzi.
Alisema tathimini inaonyesha kina mama wengi wanapendelea kutumia zaidi njia ya vipandikizi na hadi sasa huduma ya uzazi ya mpango inapatikana katika vituo vya afya 165 mkoani Geita na huduma hiyo inaendelea kufikishwa kwenye maeneo mengine kupitia kampeni ya Mkoba.
Mmoja ya waliofunga uzazi, Martha Samwel (Mama mwajuma) mkazi wa mtaa wa Miti Mirefu mjini Geita amesema ameamua kuchukua uamuzi huo ili kupata muda wa kufanya shughuli za ujasiliamalia na kulea watoto nilionao.
“Mimi nina watoto wanne, sionai haja ya kuongeza wengine wakati hawa niliona wenyewe wananitoa jasho, nikiongeza nitawaleaje mie, acha nipumunzike bhana nifanye mambo mengine,” amesema.
Alikiri hatua hiyo imemupa nafasi ya kuwahudumia watoto wake kwa ufasaha na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi kwa maana ya malazi, mavazi na chakula.