Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM |
KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Mwinyi Zahera, amesema mshambuliaji wake, Harieter Makambo, bado hajaonyesha kiwango chake, licha ya kuonyesha uwezo katika michezo miwili mfululizo.
Makambo alianza kuonyesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa kundi D katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya USM Alger, baada ya kufunga bao moja, katika ushindi wa mabao 2-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili iliyopita.
Pia mshambuliaji huyo alifunga bao moja katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania dhidi ya Mtibwa Sugar, wakati timu hiyo ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Alhamisi iliyopita.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Zahera alisema kiwango cha Makambo hapo bado na kwamba ana uwezo mkubwa na atawashangaza mashabiki wa Yanga kwa kuwapa raha kwenye ligi.
Alisema wachezaji wake walitumia nguvu nyingi katika mchezo dhidi ya USM Alger, ambao pia hawakupumzika na kukutana na Mtibwa Sugar, hali iliyosababisha wachoke kipindi cha pili.
“Nimefurahi kuona kiwango kizuri kilichoonyeshwa na wachezaji wangu, lakini vilevile katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar Makambo alichoka katika dakika 20 za mwisho, ila sikutaka kumtoa, kwani lengo langu lilikuwa ni kutaka azoee mechi ngumu na kumaliza dakika 90.
“Ukiangalia alikosa mabao kama matatu, lakini endapo angekuwa katika kiwango chake kile ninachokifahamu, naamini angeweza kufunga mabao mengine,” alisema Zahera.
Alisema Mtibwa Sugar ni timu ngumu na ina wachezaji wenye nguvu, hivyo anawapongeza nyota wake kwa kupambana hadi dakika 90 na kuweza kuibuka na pointi tatu.
Akizungumzia mchezo wa raundi ya pili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports, unaotarajiwa kuchezwa Agosti 29, mwaka huu nchini Rwanda, Zahera alisema watakwenda kucheza ili wamalize vizuri.
“Nafahamu tunakabiliwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho, lakini nguvu nyingi tunaelekeza kwenye raundi ya pili ya Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC, kwani huku hata tukishinda hatuendi kokote,” alisema.
Kocha huyo amewataka mashabiki wa Yanga kuendelea kuisapoti timu yao, kwani mipango yao ni kuwapa furaha na kupata matokeo mazuri katika michezo inayowakabili.