RAIS TRUMP KIKAANGONI, WASHIRIKA WAKE WANG’OLEWA

0
1022

NEW YORK, MAREKANI


URAIS wa Trump watikiswa. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na misukosuko ya kisiasa na kiutawala inavyoendelea nchini Marekani.

Chagizo la hali hiyo ni kutokana na vigogo kadhaa wa kambi ya kisiasa ya Rais Donald Trump ndani ya Republican kusambaratika baada ya kushtakiwa mahakamani kwa makosa mbalimbali.

Rungu hilo pia limewakuta vigogo waliokuwa wanamuunga mkono wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana ambao wamefunguliwa mashtaka ya rushwa, ufisadi na ukosefu wa maadili.

Hali hiyo imezidisha kivumbi katika utawala wa Rais huyo tangu kuingia madarakani, huku zikiibuliwa shutuma lukuki kuwa Serikali ya Urusi iliingilia mchakato wa uchaguzi mkuu huo ili kumsaidia Trump kushika wadhifa huo mkubwa.

Kuhukumiwa kwa watu muhimu katika utawala wake kumemdidimiza Rais Trump ambaye kwa muda wa miezi 19 sasa anakabiliwa na shinikizo kubwa la kung’olewa madarakani.

Kupitia makala haya tunaelezea vigogo wote waliosambaratishwa kutoka ngome ya Trump.

Baada ya miezi hiyo 19 ya mashambulizi dhidi ya Mwenyekiti wa Tume inayochunguza kuhusika kwa Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016, Robert Mueller ameanza kujibu mapigo kwa njia za kisheria baada ya vigogo hao kukutwa na hatia. Tume inayoongozwa na Mueller inaundwa na wanasheria 17 na uchunguzi wao umewashtaki watu 22 wakiwemo vigogo waliokuwa washirika wa karibu wa Rais Trump.

PAUL MANAFORT

Alikuwa Mwenyekiti wa Kampeni za Urais za Donald Trump. Msimu wa kiangazi cha mwaka 2016 ndipo tuhuma dhidi yake ziliibuliwa akidaiwa kushirikiana na bilionea mmoja mzaliwa wa Ukraine aliyekuwa ‘kibaraka’ wa Serikali ya Urusi. Tuhuma dhidi yake zilielezwa kuwa alifanya mkutano na mwanasheria wa Urusi ndani ya jengo la Trump (Trump Tower) ambako mwanasheria huyo alitoa ofa ya mchezo mchafu dhidi ya mgombea wa chama cha Democratic, Hillary Clinton.

Mahakama imemkuta na hatia katika makosa nane yakiwemo ya utakatishaji fedha, kutoa nyaraka za uongo, kuidanganya tume ya uchunguzi, kushindwa kusajili kampuni ya uwakala, kutoa nyaraka feki za kodi, kushindwa kutoa taarifa za kifedha pamoja na kuzidanganya benki mbili ili kujipatia fedha. Anakabiliwa na kifungo cha miaka 80 jela.

MICHAEL COHEN

Huyu alikuwa mwanasheria binafsi na msimamizi wa mikataba ya Trump. Ametuhumiwa kwa makosa nane yakiwamo udanganyifu wa kipato chake, ukwepaji wa kodi, kuidanganya benki ili kupata mikopo, kuvunja sheria ili kuinufaisha timu ya kampeni ya Trump, kuvunja sheria za kifedha, kuwalipa fedha wanawake waliojihusisha kimapenzi na Trump.

Mahakama ya New York imemkuta na hatia ya makosa hayo ambapo katika utetezi wake amesema alitenda hayo yote baada ya kuagizwa na mgombea wake (Donald Trump) kwa lengo la kufanya vizuri kwenye kampeni. Amehukumiwa kwenda jela miaka mitano.

RICHARD GATES

Alifanya kazi kama msaidizi wa kampeni za Trump. Ndiye alikuwa msaidizi na msiri wa Paul Manafort alipokuwa mwenyekiti wa kampeni hizo.

Gates anatuhumiwa kutenda makosa mawili Oktoba mwaka 2016 kutokana na kufanya kazi kwa siri kwa niaba ya Serikali ya Urusi nchini Ukraine na kutakatisha Dola za Marekani milioni 4 kupitia akaunti ya benki. Pia anatuhumiwa kufanya udanganyifu ili kujipatia mkopo, kutakatisha Dola milioni 30, kukwepa kodi kinyume cha sheria za Marekani, kulidanganya Shirika la Upelelezi wa ndani la FBI.

Hata hivyo Gates amesema yupo tayari kutoa taarifa za sakata la Serikali ya Urusi, hatua ambayo imechangia kuondolewa kwa baadhi ya mashtaka dhidi yake. Kwa ujumla anakabiliwa na kifungo cha miezi 71 jela, hata hivyo bado hajahukumiwa.

MICHAEL FLYNN

Flynn alikuwa mshauri wa masuala ya ulinzi wa Rais Trump. Wiki chache tangu Trump aapishwe, alitimuliwa katika wadhifa wake kwa tuhuma za kumdanganya Makamu wa Rais Mike Pence kuhusika na kuwasiliana kwake na maofisa wa Urusi.

Anatuhumiwa kulidanganya Shirika la upelelezi wa ndani la FBI katika mawasiliano yake na aliyekuwa Balozi wa Urusi, Sergey Kislyak wiki chache kabla ya Trump hajachukua madaraka rasmi.  

Naye amekutwa na hatia ya udanganyifu na kutoa ahadi ya kushirikiana na timu maalumu ya uchunguzi pamoja na kutoa taarifa sahihi za wasaidizi wengine. Anakabiliwa na kifungo cha miezi sita jela, bado hajahukumiwa hadi pale atakapomaliza kushirikiana na mwendesha mashtaka.

Jeffrey D. Gordon

Kwa mujibu wa habari zilizochapishwa na gazeti la Washington Post zimesema kuwa kigogo huyu amewahi kuwa msemaji wa Idara ya Ulinzi Pentagon kati ya mwaka 2005 hadi 2009. Alikuwa mmoja wa maofisa waandamizi wa kampeni za Trump wakati akiisaka Ikulu ya Marekani. Anatajwa kumwalika Maria Butina, mwanamke anayetuhumiwa kushirikiana na idara ya usalama ya Urusi.

Baruapepe, nyaraka na mahojiano ya Washington Post zinathibitisha kuwa Jeffrey D. Gordon ambaye alidumu kwa miezi sita akiwa mkurugenzi wa usalama wa kampeni za Trump, aliwasiliana na Maria Butina kati ya Septemba na Oktoba mwaka 2016 na kumpa mwaliko wa kuhudhuria tamasha la sherehe ya kukumbuka kuzaliwa lililohusisha bendi ya muziki wa Rock ya Styx.

Maria Butina alihukumiwa mwezi uliopita kwa kosa la kujihusisha na ujasusi kwa niaba ya Serikali ya Urusi na kuiba siri za Marekani katika vyama vya siasa na idara ya silaha.

GEORGE PAPADOPOULOS

Huyu alikuwa mshauri wa mambo ya nje wa kampeni za urais wa Trump. Alituhumiwa kwa makosa ya kulidanganya shirika la upelelezi wa ndani la FBI kuhusu mawasiliano na watu waliojitambulisha kwake kuwa ni wawakilishi wa Serikali ya Urusi pamoja na tume ya uchunguzi wa sakata hilo. Atafungwa jela miezi sita.

ALEX VAN DER ZWAAN

Van Der Zwaan ni raia wa Uholanzi na mkwe wa bilionea German Khan raia wa Urusi. Zwaan anatuhumiwa kulidanganya shirika la upelelezi wa ndani la FBI kuhusiana na kazi za usaidizi alizofanya katika kampeni za urais za Trump mwaka 2016. Amekutwa na hatia ya makosa ya kufuta ushahidi wa baruapepe, kuidanganya FBI na mwendesha mashtaka kuhusu mawasiliano ya Trump na Gates jinsi walivyoshiriki kufanya kazi na vyama vya siasa vya Ukraine vyenye masilahi na Serikali ya Urusi.

Alikuwa wa kwanza kuwekwa rumande mwanzoni mwa uchunguzi wa sakata la Urusi baada ya madai ya kuingilia uchaguzi wa Marekani. Alikaa katika gereza la Allenwood, Pennsylvania kwa siku 30, kabla ya Juni mwaka huu kurudishwa nchini Uholanzi ambako ana uraia.

DUNCAN HUNTER

Hunter alikuwa mbunge wa Bunge la Wawakilishi kutoka California, na wa pili kutangaza bayana kumuunga mkono Trump wakati alipowania urais.

Hunter na mkewe wanakabiliwa na makosa 60, ambapo walitumia Dola za Marekani 250,000 za kampeni kwa shughuli zao binafsi za mapumziko, karo za shule na matibabu ya meno. Ingawaje Hunter ni miongoni mwa wagombea wa nafasi hiyo na jina lake litatokea kwenye karatasi za kura Novemba mwaka huu dhidi ya Ammar-Campa Najjar, bado ana wakati mgumu kwa mashtaka yanayomkabili.

CHRIS COLLINS

Ni mbunge wa Bunge la Wawakilishi kutoka New York na alikuwa wa kwanza kutoka huko kumuunga mkono Trump katika harakati zake za urais. Anatuhumiwa makosa ya kuwadanganya mawakala wa shirika la upelelezi wa ndani la FBI, udanganyifu wa taarifa za tiba za kampuni Immunotherapeutics na kumpa mtoto wake. Alikamatwa Agosti 8, mwaka huu.

TAASISI YA TRUMP

The Trump Organization ni mali ya Donald Trump ambayo hujihusisha na shughuli za kijamii. Mwanasheria wa jijini New York, Barbara Underwood alifungua kesi dhidi ya taasisi hiyo Juni mwaka huu, kwamba ilivunja sheria kwa kujihusisha na matukio ya kisiasa kinyume cha  usajili wake, kushiriki kampeni za urais za Trump na kushindwa kutekeleza sheria za fedha.

Ofisi ya mwanasheria wa New York iliomba mahakama kumlazimisha Trump na familia yake kulipa faini ya Dola milioni 2.8 za Marekani, kwa upande wake Rais Trump amepuuza jambo hilo na kuliia la ajabu.

WARUSI 12

Maofisa 12 wa idara ya usalama ya Serikali ya Urusi wametajwa kuwa miongoni mwa vigogo waliomsaidia Trump kuingia madarakani.

Tume ya uchunguzi ilisema walikuwa wanatekeleza operesheni maalumu ya Serikali ya Urusi kwa lengo la kutengeneza ushawishi matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016.

Wametuhumiwa makosa 11 ikiwemo kuingilia taarifa za ndani za Chama cha Democratic zikiwemo baruapepe za Hillary Clinton katika ofisi binafsi. Februari mwaka huu maofisa 13 wa Urusi na wafanyabiashara watatu pamoja na taasisi ya masuala ya mtandao wa Intaneti walikuwa ‘mawakala’ wa Serikali ya Urusi waliofanikisha kuiba nyaraka mbalimbali za Marekani.

Hata hivyo, Marekani imeshindwa kuwafungulia kesi kwa kuwa wote walifanikiwa kurejea nchini kwao Urusi hivyo hawatahukumiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here