Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
HOMA ya pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga, litakalochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, linazidi kupamba moto.
Mchezo huo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania kwa msimu wa 2018/19 kwa wakongwe hao kukutana, unatarajiwa kuanza saa 10 jioni, ukichezeshwa na mwamuzi mzoefu, Jonesia Rukyaa, kutoka Kagera.
Mwamuzi huyo wa kati, atasaidiwa na Ferdnand Chacha kutoka Mwanza na Mohammed Mkono wa Tanga, wakati mwamuzi wa mezani akiwa Elly Sassi wa Dar es Salaam.
Kocha mkuu wa timu ya Yanga, Mwinyi Zahera, akizungumzia mchezo huo jana, alisema ataangalia video mbili za mchezo wa watani wao kabla ya kuvaana nao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Zahera, alisema wataangalia na wachezaji wake video hizo ili wafahamu mfumo ambao wanatumia ili iwe rahisi kukabiliana nao.
“Tunaendelea na mazoezi na kuwapanga wachezaji wangu jinsi na namna ya kukabiliana na wapinzani wetu, ikiwa ni pamoja na kukaa pamoja kuangalia video kama mbili ili tuweze kufahamu mfumo wanaotumia,” alisema.
Alisema maandalizi yao yapo kawaida kama ilivyo michezo mingine kwani watacheza kwa umakini zaidi ili wasifanye makosa yoyote.
Naye kocha mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, alisema wanafanya maandalizi kama ilivyokuwa kwa michezo mingine kwa kuwa wanakutana na timu ambayo nayo inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kama ilivyokuwa wao.
Alisema wameamua kupotezea kambi ya Zanzibar na kusalia Dar es Salaam tofauti na ilivyozoeleka ambapo mara nyingi wamekuwa wakiweka kambi visiwani humo, kwani mchezo huo ni kama ilivyokuwa mingine.
“Nimeamua kuweka kambi hapa hapa kwani hakuna tofauti ya kwenda sehemu nyingine, ukiangalia maandalizi tunayofanya ni ya kawaida licha ya kuwa mashabiki wanachukuliwa tofauti,” alisema.
Alisema alimwacha Dar es Salaam msaidizi wake, Masoud Djuma, kwa mechi tatu za ugenini ili aweze kuendelea na majukumu mengine ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia wapinzani wao Yanga na sasa wanayafanyia kazi.
“Kwa sasa naendelea na maandalizi na kuyafanyia kazi baadhi ya mapungufu kwa wachezaji wangu, ambao kwa sasa kila mmoja ana morali ya juu, licha ya kuwa tutamkosa John Bocco, ambaye ana kadi nyekundu ila wapo wengine ambao wataziba pengo hilo,” alisema.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa msimu uliopita, ambapo walitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, wakati waliporudiana Yanga walifungwa bao 1-0, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.