*Yampa Lwandamina mara mbili ya mshahara wa Zesco
*Ruksa kusajili mchezaji yeyote anayemtaka
Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, imeamua kufanya kufuru kwa kuvunja benki ili kumnasa kocha Mzambia, George Lwandamina, aliyeifikisha Zesco United nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti la MTANZANIA limezipata kutoka Zambia, zinadai kuwa Lwandamina alikuwa akilipwa mshahara wa dola 4,000 (Sh milioni 8.2) kwa mwezi katika klabu ya Zesco, dau ambalo Yanga wamekubali kutoa mara mbili yake ili kumleta nchini kocha huyo.
Lwandamina ambaye alitua nchini Jumapili mchana kwa ajili ya kumalizana na uongozi wa Yanga, anatarajiwa kurithi mikoba ya kocha wa sasa wa timu hiyo, Hans van der Pluijm, ambaye mshahara wake ni dola 10,000 (Sh milioni 22.2).
Kabla ya kuchagua kuja kuifundisha Yanga, Lwandamina alikuwa na ofa kibao mezani kwake ikiwemo moja kutoka katika klabu ya Free States ya Afrika Kusini, lakini pia timu yake ya Zesco ilikuwa inataka kumuongezea mkataba, lakini alizikataa ofa zote hizo baada ya kuona dau lililowekwa mezani na miamba hiyo ya Jangwani.
Inaaminika kuwa Yanga imemwekea Lwandamina dau kama analolipwa Pluijm anayetarajiwa kupewa jukumu la Ukurugenzi wa Ufundi katika klabu hiyo ya Jangwani, ndiyo maana imekuwa ngumu kwake kukataa kwa sababu ni mara mbili ya mshahara wake aliokuwa akichukua Zesco.
Wakati huo huo; MTANZANIA lina taarifa kuwa tayari Lwandamina ameshasaini kwa siri kubwa mkataba wa miaka miwili kuifundisha klabu hiyo ya Jangwani, katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
MTANZANIA lina taarifa kuwa katika mkataba huo, Lwandamina amepewa uhuru wa kusajili mchezaji yeyote atakayemtaka tena kwa gharama yoyote, lakini pamoja na uhuru huo, klabu imembana kocha huyo na kipengele ambacho kinaweka wazi kuwa lazima aifikishe timu angalau kwenye nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Inasemekana Lwandamina aliyewahi kukinoa kikosi cha timu ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’, ameletwa Yanga ikiwa ni sehemu ya mchakato wa Kampuni ya Yanga Yetu Limited kukiboresha kikosi cha timu hiyo ambayo wataikodisha kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.
Maboresho ya benchi la ufundi la Yanga yatafanywa pia kwa wasaidizi wa Pluijm ambao ni kocha msaidizi, Juma Mwambusi, kocha wa makipa, Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh.
Nafasi za wasaidizi wa Pluijm zimetajwa kujazwa na wazalendo, Charles Boniface Mkwasa ambaye atakuwa kocha msaidizi, Manyika Peter, kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.
Habari zaidi za ndani zinadai kuwa mara baada ya klabu kumalizana na Lwandamina, uongozi sasa una mtihani wa kumshawishi Pluijm achukue jukumu jipya la Ukurugenzi wa Ufundi, lakini ikiwa atagoma inadaiwa kuwa tayari umejipanga kuleta mtaalamu kutoka Ureno kufanya kazi hiyo.
Lakini, wakati Yanga ikiendelea kumshawishi Pluijm kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo, kuna taarifa kuwa Mholanzi huyo anawindwa na klabu ya Azam FC, ambayo imeanza vibaya msimu huu chini ya kocha Mhispaniola, Zeben Hernandez.
Yanga ambayo mwaka huu iliishia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, imeamua kumleta Mzambia huyo kutokana na mafanikio aliyoipa Zesco kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, ambapo aliifikisha timu hiyo nusu fainali ya michuano hiyo.
Katika nusu fainali ya michuano hiyo, Zesco walitolewa na mabingwa wa Afrika, Mamelod Sundown ya Afrika Kusini kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-2 dhidi ya Zamalek, hii ni baada ya kushinda nyumbani 2-1 na kukubali kichapo cha mabao 2-0 ugenini.
Rekodi nzuri ya Lwandamina Afrika ndiyo imeuvutia uongozi wa Yanga kumleta kocha huyo ambaye kwenye hatua ya makundi la Ligi ya Mabingwa Afrika, alizichapa bila huruma timu za Uarabuni ikiwemo Al Ahly ya Misri.
Katika hatua nyingine, Lwandamina tayari ameshaanza harakati za kuimarisha kikosi cha Yanga na taarifa kutoka Zambia zinadai kuwa tayari mastaa wawili wa Zesco United, wako njiani kuja Jangwani kwenye usajili wa dirisha dogo.
Mastaa hao kutoka Zambia ni pamoja na straika, John Ching’andu, kiungo mchezeshaji fundi, Cletus Chama Chota na beki mmoja, ambao wanatarajiwa kumalizana na Yanga wakati wowote kutoka sasa ili waje Jangwani kuungana na kocha Lwandamina kwenye harakati za kuhakikisha wanaifikisha timu hiyo mbali zaidi kwenye michuano ya Afrika.