THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Yanga, umesema una uhakika wa kuwatandika watani wao wao wa jadi, Simba, lakini umewataka waamuzi kuhakikisha wanachezea kwa haki bika upendeleo.
Yanga na Simba zinatarajia kushuka dimbani kuumana , katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Marchi 8 mwaka huu, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Timu hizo zilipokutana katika mchezo wa kwanza matokeo baada ya dakika tisini kukamilika yalikuwa sare ya mabao 2-2.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Alliance ambao Wanajagwani walishinda mabao 2-0 juzi Uwanja wa Taifa, Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugas, alisema safari hii hawatafanya makosa ya mchezo wao kwanza zaidi ya kupata ushindi dhidi ya wapinzani wao hao.
“Tumejipanga vizuri , tuna uhakika tutapata ushindi mnono nachowaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi katika mchezo huu ukizingatia sisi ndio tutakuwa wenyeji.
“Lakini pamoja na yote tunawaomba Waamuzi watakaopangwa wachezeshe kwa haki ili mshindi apatikane kwa haki,” alisema.
Alisema dalili nzuri imeanza kuonekana katika mchezo uliopita dhidi ya Alliance ambao walipata ushindi wa mabao 2-0, hivyo wanaamini burudani hiyo kuendelea kwa mara nyingine.
Nugas aliwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia ufundi utakaonyeshwa na wachezaji wao wakiwemo Benard Morrison ambaye amekuwa akionyesha kiwango kizuri katika mechi zao.