MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
YANGA imepiga kambi ya muda mfupi jijini Lusaka, Zambia kabla ya kuwafuata wapinzani wao Zesco United katika Mji wa Ndola.
Timu hizo zitashuka dimbani Jumamosi hii kuumana, katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Jumamosi hii mjini Ndola.
Kutoka Lusaka iliyo Yanga hadi Ndola utakaopigwa mtanange huo ni umbali wa kilometa 320 (sawa na maili 171). Kwa mwendo wa kawaida wa gari umbali huo utatumia si chini ya saa mbili.
Msafara wa wachezaji 22 na viongozi saba wa benchi la ufundi uliondoka jana kwa mafungu mawili, kundi la kwanza la wachezaji 10 liliondoka mapema asubuhi, huku la pili likiondoka saa 2:00 usiku kuwafuata vijana hao wa George Lwandamina.
Uongozi wa Yanga umeamua kikosi chao kitulie kwanza Lusaka na kuendelea na mikakati yao ya kuwakabili wapinzani wao kabla kesho kuelekea Ndola tayari kwa mchezo huo.
Awali kikosi hicho kilipanga kutua moja kwa moja mjini Ndola utakapochezwa mchezo huo, lakini baada ya kupima upepo wameibani kuwa lazima timu hiyo ijifiche Lusaka na kusuka mikakati ya ushindi.
Katika mchezo wa awali uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1,hivyo Yanga inahitaji ushindi wowote au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili kutinga hatua makundi.
Wachezaji watakaowakosa Zesco ni na mabao hawajasafiri kwenda Zambia ni Paulo Godfrey, Mapinduzi Balama na Issa Bigirima ambao wanasumbuliwa na majeraha, huku David Molinga na Selemani Moustafa wakisalia nchini kutokana na kutokuwa na leseni za kucheza michuano hiyo zinazotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Kwa kufahamu uzito wa kazi iliyo mbele yao, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela alitua Zambia tangu juzi kwa lengo la kuweka mazingira sawa ili kikosi hicho kitakapotua huko basi kisipate bugudha yeyote ya nje ya uwanja.
Akizungumza na MTANZANIA jana Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, Rogers Gumbo alisema kikosi chao kimekamilisha maandalizi ya kwa ajili ya kuhakikisha wanapindua matokeo.
“Maandalizi ya safari yamekamilika kwa kiasi kikubwa na msafara wa timu umeanza kuelekea Zambia lakini tutafikia Lusaka na kuweka kambi ya muda kabla ya kwenda Ndola, tumeamua kufikia hapo ili tufanye maandalizi ya mwisho kabla ya kwenda huko.
“Ni kweli awali tulipanga kutua moja kwa moja Ndola lakini tumeamua kubadili mipango hiyo kutokana na ripoti tuliyopewa na watu waliotangulia huko timu sasa itakwenda Ndola Alhamisi ,”alisema.
Alisema kuwa msafara mwingine wa viongozi na mashabiki wa klabu hiyo utaanza kesho kwenda moja kwa moja Ndola kuisapoti timu yao.