Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Sasa ni rasmi kuwa Yanga SC wametwaa Ubingwa Michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa jumla wa Penalti 4-3 baada ya sare ya 0-0 dhidi ya Simba SC katika dakika 90 za mchezo huo wa fainali uliopigwa kwenye dimba la Amaan visiwani Zanzibar.
Katika dakika 90 Watani wa Jadi, Yanga SC na Simba SC walipepetana vikali licha ya kosa kosa za hapa na pale na kutoa sare ya 0-0 mbele ya mashabiki lukuki katika Uwanja wa Amaan.
Kwa ubingwa huo Yanga SC wanatwaa taji na kitita cha Sh milioni 15 kibindoni na medali za dhahabu.
Golikipa wa Yanga SC, Farouk Shikhalo ndiye aliyekuwa bora zaidi katika Mikwaju ya penalti akidaka Penalti moja ya nne iliyopigwa na beki wa Simba SC, Joash Onyango Achieng sambamba na hilo, mshambuliaji wa Yanga SC, Saido Ntibazonkiza alipiga penalti ya mwisho iliyoipa ubingwa Yanga SC katika Penalti hizo.
Simba SC washindi wa tatu wameambulia medali sambamba na kitita cha Sh milioni 10. mfungaji bora wa mshindano ni mshambuliaji wa Simba SC, Miraji Athumani, Kiungo wa Simba SC, Francis Kahata ameibuka kuwa mchezaji Bora wa Mashindano na Farouk Shikhalo wa Yanga SC golikipa bora wa michuano.