NA CLARA ALPHONCE
KLABU ya Yanga kwa kauli moja imethibitisha kuwa itafanya uchaguzi wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi Januari 13 mwakani, ilivyotakiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini imeendelea kupinga mchakato huo kusimamiwa na taasisi hiyo.
Kutokana na msimamo huo, klabu hiyo imeunda kamati yake ya uchaguzi ya watu saba ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia mchakato mzima.
Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Siza Lyimo, aliitangaza kamati hiyo jana mbele ya viongozi wa matawi 60 ya klabu hiyo yaliyohudhuriwa na mkutano wa dharura.
Mkutano huo ulifanyika makao makuu ya klabu hiyo yaliyoko mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.
Kamati hiyo inaongozwa na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Jabir Katundu, wengine ni Samwel Mapende, Daniel Mbelwa, Mustaphar Nagari, Wakili Godfrey Mapunda, Wakili Edwin Mwakingu na Samwel Mangesha.
Lyimo alisema fomu za uchaguzi zitaanza hivi karibuni makao makuu ya klabu hiyo.
Wakati huo huo, Kamati ya Utendaji ya Yanga imemteua Samwel Lukumay kuwa kaimu mwenyekiti wa klabu hiyo na Lyimo kuwa makamu Mwenyekiti.
Pia ilimteua Hussein Nyika kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ambaye anaungana na wajumbe wengine watatu ambao hawakujiuzulu nafasi zao.
Alisema viongozi hao wataiongoza Yanga hadi pale watakapopata viongozi wapya kupitia uchaguzi wao wa kujaza nafasi.
Kuhusu sababu zilizosababisha mkutano mkuu wa dharura wa klabu hiyo kutofanyika jana kama walivyopangwa awali, alisema ilitokana na Jeshi la Polisi kuuzuia, baada ya kubaini kuna baadhi ya wanachama wa klabu hiyo walipanga kufanya vurugu.
Alisema Mkutano huo, utapangiwa tarehe nyingine mara baada ya vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kujiridhisha kuwapo kwa hali ya amani.
Awali ulitanguliwa mkutano wa viongozi wa matawi, ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kanda ya Kinondoni, Shabaan Mgonja.
Mkutano huo ulikuwa na ajenda mbili, moja ikiwa ni kutaka kupewa sababu za kuahirishwa kwa mkutano wa jana ambao ulipangwa kufanyika Viwanja vya PTA na uchaguzi.
Katika mkutano huo, viongozi wa matawi walilialika Baraza la Wadhamini na Kamati ya Utendaji ya Yanga.
Kwa pamoja viongozi hao waliendelea kupinga uchaguzi wao kusimamiwa na TFF, wakidai ni kinyume na Katiba ya Yanga.
Mgonja alisema katiba yao ya mwaka 2011 hairuhusu taasisi au mamlaka yoyote kusimamia uchaguzi wa Yanga, badala yake kazi hiyo itafanywa na Wanayanga wenyewe.