23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga wapiga darasa Uturuki

yanga sc
yanga sc

* Bossou kuifuata timu leo, Cannavaro kutocheza Algeria

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa timu ya Yanga, jana wameendelea na mazoezi nchini Uturuki huku kocha wa timu hiyo, Hans Van De Pluijm, akiendesha darasa kuwapa mbinu kali za kuwaua wapinzani wao katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Yanga imepiga kambi katika hoteli kali ya Rui mjini Antalya, Uturuki kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia Juni 19, mwaka huu, utakaofanyika Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria.

Taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo zinadai kuwa timu hiyo inafanya mazoezi asubuhi na jioni, huku katika muda wa ziada wachezaji wanaingia darasani kwa ajili ya kufundishwa na walimu wao.

“Yanga ipo katika kambi makini, nia ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo yetu ili tuweke historia kila mchezaji anaonekana yupo vizuri wakifuata maagizo ya mwalimu.

“Hakutakua na mechi yoyote ya kirafiki labda mwalimu atake mwenyewe,” kilisema chanzo hicho kutoka Uturuki.

Wakati huo huo, beki wa kati wa timu hiyo, Vincent Bossou, anatarajia kujiunga na wenzake leo nchini Uturuki.

Bossou hakufanikiwa kuondoka na kikosi cha Yanga juzi alfajiri kilichoelekea Uturuki, kutokana na kuchelewa kurejea nchini baada ya mapumziko kwa  madai ya kuwa na matatizo ya kifamilia.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo ilisema kuwa awali beki huyo alitakiwa aungane na timu hiyo moja kwa moja Algeria baada ya kumaliza matatizo yake ya kifamilia.

“Yanga pia itamkosa beki wake tegemeo wa kulia, Juma Abdul kwa wiki mbili kwa sababu ya kuumia kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Mei 25 mwaka huu Yanga iliposhinda 3-1.

“Kutokana na tatizo hilo huenda Hassan Kessy, akachukua nafasi yake pia mbali na Juma Abdul, wengine walioachwa ni Malimi Busungu, kipa Benedictor Tinocco na mshambuliaji, Paul Nonga ambao hawamo kwenye programu ya kocha wakati kinda Yussuf Mhilu hatakwenda kwa sababu jina lake halijasajiliwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF),” kilisema chanzo hicho.

Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisafiri na timu hiyo lakini inasemekana kwamba hatacheza mechi hiyo ya kwanza ya Kundi A kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo uliopita dhidi ya Sagrada Esperanca nchini Angola.

Kiungo Salum Telela ni mchezaji pekee aliyemaliza msimu na Yanga ambaye hakusafiri kwa sababu hajapewa mkataba mpya baada ya kumalizika wa awali.

Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli, Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles