26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA VS PRISONS LEO NI HESHIMA NA KISASI

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

KIKOSI cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo kitashuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya wapinzani wao, Tanzania Prisons, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Yanga kama itafanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo, itafikisha pointi 23 na kuwashusha mahasimu wao, Simba, walioko kileleni wakiwa na pointi 22, sawa na Azam FC, walioko nafasi ya pili kutokana na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Lakini kama vijana hao wa Jangwani watapata sare au kupoteza mchezo wa leo wanaweza kujikuta ikitengeneza pengo kubwa zaidi kati yake na Simba endapo kesho itavuna ushindi kwenye Uwanja wa Uhuru dhidi ya Lipuli FC na Azam, ambayo Jumatatu itakabiliana na Mtibwa Sugar.

Yanga ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 20, walizozipata baada ya kucheza michezo 10, wakishinda mitano na kutoka mechi tano sare tano.

Katika mchezo huo, Yanga itataka kuendeleza ubabe wao baada ya kuibuka na ushindi mnono wa bao 5-0 wiki iliyopita dhidi ya Mbeya City, Uwanja wa Uhuru.

Hata hivyo, rekodi za msimu uliopita kati ya timu hizo zinaibeba Yanga kuelekea mchezo wa leo.

Rekodi hizo zinaonyesha Yanga iliibuka na ushindi katika michezo yote miwili, ikipata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Sokoine, kisha ikashinda mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Lakini kitendo cha kupoteza pointi sita katika mechi zake mbili mfululizo zilizopita kitaifanya Prisons kupambana kwa nguvu ili kuizamisha Yanga na kuvuna pointi tatu.

Askari Magereza hao walianza kwa kuchapwa mabao 2-1 na Kagera Sugar, kabla ya kubamizwa bao 1-0 na Simba wiki iliyopita.

Matokeo hayo yameifanya ishike nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 14, baada ya kucheza michezo 10, ikishinda mitatu, sare tano na kupoteza miwili.

Kikosi cha Yanga kitaimarika zaidi baada ya kurejea kwa mpachika mabao wao hodari, Mrundi Amis Tambwe, ambaye alikosa michezo mingine yote ya timu hiyo msimu huu kutokana na kuwa na majeruhi.

Yanga itaendelea kukosa huduma za viungo Papy  Tshishimbi na Thabani Kamusoko, ambao bado wanasumbuliwa na majeraha.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, aliliambia MTANZANIA ataingiza kikosi chake uwanjani akiwa na lengo la kuvuna ushindi mkubwa.

“Utakuwa mchezo mgumu, kwani hata wapinzani wetu wamejipanga vizuri, malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda michezo yote ili kufanikisha kutetea taji letu,” alisema Lwandamina.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Prisons, Abdallah Mohamed, alisema kikosi chake kipo imara kuhakikisha kinapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo.

“Hatuna hofu juu ya kilichowakuta Mbeya City, tumejipanga vizuri kuhakikisha haturudii makosa tuliyofanya katika michezo yetu miwili iliyopita.

“Tumefanya maandalizi ya kawaida kama ambavyo tumekuwa tukifanya tunapocheza na timu nyingine, lakini Yanga wasitarajie mteremko, wajipange,” alisema Mohamed.

Ligi hiyo itaendelea kutimua vumbi pia kwenye  viwanja vingine vine. Kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, Majimaji watakuwa wageni wa Ruvu Shooting, Kagera Sugar itakuwa mwenyeji wa Stand United kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Mbao FC itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuumana na Mwadui FC, Mbeya City itakuwa kwenye Uwanja wa Namfua kupepetana na na wenyeji wao, Singida United.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles