27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 8, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

YANGA SHWARI KWA RUVU SHOOTING

NA WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM

TIMU ya Yanga imeendelea kuwapa raha mashabiki wake, baada jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Bao pekee la  Yanga kwenye mchezo huo, lilifungwa dakika ya 40 kwa kichwa na mshambuliaji David Molinga.

Molinga sasa amefikisha idadi ya mabao saba aliyoifungia Yanga msimu huu.

Kinara wa mabao mpaka sasa ni mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere ambaye amefunga mara 12.

Kwa ushindi wa jana dhidi ya Shooting, Yanga imelipa kisasi  baada ya kulazwa bao 1-0  na wanajeshi hao wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kati ya timu hizo uliochezwa pia kwenye uwanja huo.

Pia ushindi wa jana uliifanya Yanga kufikisha pointi 37 na kusalia nafasi ya tatu, baada ya kucheza michezo 18, ikishinda 11, sare nne na kupoteza mara tatu, ikiwa nyuma ya vinara Simba iliyoko kileleni na pointi zake 50, kupitia michezo 20 iliyoshuka dimbani, ikishinda 16, sare mbili na kupoteza mbili.

Nafasi ya pili ipo Azam yenye pointi 41, baada ya kushuka dimbani mara 20, ikishinda michezo 12, sare tano na kupoteza mara tatu.

Mchezo ulianza kwa Yanga kuutawala mchezo na kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Shooting.

Dakika ya 15, pasi safi ya Papy Tshishimbi ilimkuta Molinga, lakini mpira wa kichwa alioupiga kwa ufundi ulipanguliwa na kipa wa Shooting, Mohamed Makaka.

Dakika ya 25, mkwaju wa Benard Morrison ulipanguliwa na Makaka.

Wakati wote huu, Shooting ilionekana kukosa mbinu sahihi za kuipenya safu ya ulinzi ya Yanga iliyokuwa chini ya beki kisiki, Lamine Moro.

Dakika ya 32, Tshishimbi alipokea pasi safi ya Haruna Niyonzima, lakini mkwaju wake dhaifu ulidakwa na Makaka.

Dakika ya 37, mshambuliaji wa Yanga, Ditram Nchimbi alionyeshwa kadi ya njano  na mwamuzi wa mchezo huo, Rafael Ilambi wa Morogoro, baada ya kumfanyia madhambi Shaaban Kisiga wa Shooting.

Dakika ya 39, mshambuliaji Fully Maganga alikaribia kuifungia Shooting, lakini mpira wake wa kichwa ulidakwa na kipa wa Yanga, Metacha Mnata.

Mkakati wa Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael ulizaa matunda dakika ya 40 baada ya pasi nzuri ya Nchimbi kumkuta Molinga ambaye aliunganisha wavuni mpira kwa kichwa na kuwapa Wanajangwani hao bao la uongozi.

Bao hilo lilidumu hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zilipokamilika.

Kipindi cha pili, Shooting ilionekana kuamka na kuutawala mchezo.

Dakika ya 57, Kocha Mkuu wa Shooting, Salum Mayanga, alimtoa William Patrick na kumwingiza Shaaban Msala.

Dakika ya 62, Graham Naftari aligongesha mwamba wa juu wa Yanga kabla ya mpira kurudi uwanjani.

Dakika ya 68, Tshishimbi alilimwa kadi ya njano kwa kumchezea madhambi Maganga.

Dakika ya 69, Eymael alimtoa Molinga na kumwingiza Yikpe Gislain.

Dakika ya 79, Baraka Mtui wa Shooting alilimwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Morrison.

Dakika ya 80, Yikpe alishindwa kutumia vema pasi ya Nchimbi kuifungia Yanga bao la pili, baada ya kupiga shuti dhaifu lililodakwa na Makaka.

Dakika ya 81, Eymael alimtoa Morrison na kumwingiza Deus Kaseke.

Pamoja na mabadiliko yaliyofanywa na kila upande, dakika 90 zilikamilika kwa Yanga kutakata kwa bao 1-0.

Matokeo ya michezo mingine iliyopigwa jana, Azam ilishinda mabao 3-1 dhidi ya KMC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Mbao na Alliance zikatoka sare ya bao 1-1, Coastal Union ikaitandika Polisi Tanzania mabao 2-1.

Mwadui ikatoka sare ya mabao 2-2 na Singida United, Mbeya City ikaishinda Prisons bao 1-0, Kagera Sugar ilatoka suluhu na Biashara United, wakati Lipuli ikaitungua Mtibwa Sugar bao 1-0.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles