NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
KLABU ya Yanga, imeendelea kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao, baada ya kumnasa kiungo Mapinduzi Balama, kwa kumsajili kwa mkataba wa miaka mitatu.
Balama alijiunga na Yanga, baada ya kung’ara na kikosi cha timu ya Alliance FC ya Mwanza aliyoichezea msimu uliopita.
Mchezaji huyo, ataungana na wakali wengine wapya ambao wamethitishwa kusajiliwa na Wanajagwani hao ambao ni
, mshambuliaji, Balinya Juma kutoka Polisi ya Uganda, beki wa kati, Lamine Moro kutoka Ghana, Patrick Shibomana kutoka Rwanda, Mustafa Selemani kutoka Burundi na Abdulazizi Makame aliyemaliza mkataba katika klabu ya Mafunzo ya Zanzibar.
Wengine ni beki, Ally Ally kutoka KMC, na mshambuliaji, Sadney Urikhob raia wa Namibia.
Balama alithibitishwa rasmi jana kuichezea Yanga msimu ujao, kupitia taarifa iliyotolewa katikia mtandao rasmi wa klabu hiyo.
Usajili huo ni mapendekezo ya kocha, Mwinyi Zahera ambaye ametaka wasajiliwe wachezaji wa kiwango cha juu, watakaoirudisha timu hiyo katika makali yake na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulitua kwa watani zao, Simba kwa misimu miwili mfululizo.