NA AYOUB HINJO
MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulianza Agosti 26, kwa kila timu kucheza mchezo wake wa ufunguzi, lakini Yanga walitupa karata yao siku iliyofuata kwa kucheza na Lipuli kutoka Iringa.
Mchezo uliisha kwa sare ya bao 1-1, huku Lipuli wakionekana kupata walichokihitaji kutoka kwa Yanga. Mara nyingi ni ngumu timu ndogo kujilipua kushambulia dhidi ya timu kubwa.
Walichofanya ni kukaa nyuma ya mpira kisha kutumia mipira mirefu kufanya mashambulizi, hakika walifanikiwa kwao ni faida kubwa.
Udhaifu ulionekana kwa Yanga kushindwa kuvunja mitego ya Lipuli. Walionekana wanacheza tu, hawakuwa sawa katika ubora wao wa kutambua udhaifu wa mpinzani wao.
Bado inakuwa ngumu kwao labda mchezo unaofuata dhidi ya Njombe Mji waingie na mbinu mpya kesho, sababu kilichotokea dhidi ya Lipuli kinaweza kutokea tena katika Uwanja wa Sabasaba.
Njombe Mji kwa uhakika watajilinda kama Lipuli, hilo linajulikana. Je, Yanga wataweza kutegua mtego huo na kuondoka na ushindi? Hilo ndilo swali linaloumiza vichwa vya mashabiki wao.
Kila mmoja anaonekana kuwa na mashaka na kikosi cha Yanga kwa sasa, labda inawezekana kutokana na matatizo ya ukata yaliyoikumba timu hiyo hivi karibuni.
Sidhani kama tatizo hilo bado linaendelea, naamini watakuwa wamekwisha malizana na wachezaji wao wote ili kuuanza msimu wakiwa na kitu kipya chenye manufaa zaidi kwa timu yao.
Aina ya kikosi chao cha sasa ni tofauti kidogo na kilichotumika msimu uliopita. Hawana Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, pia hawana makipa wao bora wawili, Deogratius Munishi na Ally Mustafa.
Ramadhani Kabwili, Maka Edward, Said Hamisi, Abdalah Shaibu, Yusufu Mhilu, Gadiel Michael, Ibrahim Ajib na Rafael Daudi ni baadhi ya wachezaji ambao wameonekana kwenye kikosi hicho kabla ya msimu kuanza.
Huku gumzo la jiji akiwa Papy Kabamba Tshishimbi kutoka Congo DR, sihitaji kumwelezea sana Tshishimbi sababu kila mmoja aliona alichokifanya dhidi ya Simba. Ni usajili bora uliofanywa na Yanga.
Bado wanaonekana hawajakamilika, timu yao kuna vitu wanakosa labda kutokana na majeruhi ya baadhi ya nyota au nafasi za walioondoka hazijazibwa kikamilifu.
Wanakosa huduma ya Amissi Tambwe, sababu ya majeruhi, hakika pengo lake linaonekana, timu imeshindwa kuziba nafasi sababu wamekosa mmaliziaji mzuri wa nafasi ambazo wanazitengeneza.
Donald Ngoma si mshambuliaji wa mwisho kwa asili, mfumo ambao unatumiwa sasa si rafiki kwake. Muda mwingi anajikuta yupo nje ya majukumu yake, sababu si mshambuliaji tegemeo.
Kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, aliwahi kusema “washambuliaji wanakufanya ushinde mchezo lakini mabeki wanakufanya ushinde ubingwa”.
Ni kweli kabisa, bila safu imara ya ushambuliaji huwezi kushinda mchezo ambao utakufanya usogelee ubingwa kwa urahisi. Safu imara ya ulinzi inakufanya umalize mchezo ukiwa na uhakika zaidi wa kushinda ubingwa.
Kwa timu ya Yanga, bado wana tatizo la ulinzi kwa sasa. Hawana mabeki imara wa kati, kiasi cha kumfanya kiungo wao mkabaji, Tshishimbi kucheza chini sana.
Kevin Yondani na Nadir Haroub wanaelekea ukingoni, hawa ni mabeki bora kabisa hapa nchini lakini jua linazama wanahitaji kucheza michezo michache ili kukupa unachokihitaji.
Andrew Vincent na Abdallah Shaibu, wanahitaji kucheza michezo mingi ili kujenga ukuta imara na maelewano mazuri. Tatizo wote wanaonekana bado wanahitaji kiongozi ili wacheze vizuri.
Njia rahisi ya kuwasaidia wachezaji hao ni kuwachezesha kando ya Yondani au Nadir ili kupata uzoefu kutoka kwa wakongwe hao. Endapo hilo likifanikiwa kwa asilimia kubwa timu hiyo itakuwa na uhakika wa mabeki imara kwa miaka ijayo.
Ukiacha nafasi ambazo zimeachwa na wachezaji walioondoka, bado hata hawa waliosajiliwa bado hawajaingia moja kwa moja kwa viwango vizuri. Jambo muhimu kwao ni muda tu.