27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga kumburuza Okwi FIFA

Emmanuel Okwi
Mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Yanga, Emmanuel Okwi

NA ZAITUNI KIBWANA, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa timu ya Yanga unakusudia kuwasilisha malalamiko yao katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kupinga Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kumuidhinisha Okwi kuichezea Simba.

Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Richard Shinamkutwa, ilikutana juzi kujadili usajili huo uliozua utata na kumuidhinisha Okwi kama mchezaji huru, akiwemo beki, Abdi Banda wa Coastal Union, aliyeidhinishwa pia kuichezea Simba.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwanasheria wa Yanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ndogo za klabu hiyo, Sam Mapande, alisema wanakata rufaa maamuzi yaliyotolewa na TFF.

Alisema lengo la kwenda FIFA ni kutafuta haki yao waliyoshindwa kuipata TFF, baada ya kukiuka kanuni za maadili yaliowekwa na FIFA.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya FIFA, kipengele cha 19 (2) kinachozungumzia juu ya mgongano wa kimaslahi, mtu yeyote anayefanya kazi inayotambulika na shirikisho hilo, hapaswi kuhusika kwa lolote kutoa uamuzi katika suala linalogusa maslahi yake binafsi, familia, ndugu, rafiki au kitu chochote kinachomuhusu.

Kipengele hicho kinaweka wazi kuwa iwapo mtu yeyote atahusika katika maamuzi ya suala ambalo ana maslahi nalo, italazimika kuripotiwa FIFA ili shirikisho hilo liweze kuchukua hatua juu ya hilo.

Mwanasheria huyo aliyeongozana na msaidizi wake, Onesmo Mpinzile, alisema Mwenyekiti wa Kamati ya usajili wa klabu ya Simba, Zacharia Hanspope hakupaswa kuingia katika kikao hicho kwa kuwa tayari alikuwa na mgongano wa kimaslahi.

“Tulipoingia kwenye kikao tu tuliomba Hanspope atoke kwenye kikao hicho, ila Mwenyekiti Richard Shinamkutwa akiwa na wajumbe Abdul Sauko, Phelemon Ntahilaja na Moses Kaluwa ila hawakutusikiliza na kukiuka katiba ya FIFA,” alisema.

Alisema pia kesi yao ya msingi walizowasilisha TFF tangu Juni 27 na 23 Agosti, hazikusikilizwa na badala yake kamati hiyo ilianzisha hoja isiyokuwepo.

Alisema Okwi hakupeleka madai TFF, hivyo wanashangaa kamati hiyo kwa kuanza kujadili hoja ya mkataba wakati haikuwepo kwenye malalamiko yao.

Aliwataka mashabiki wa timu hiyo kutulia kwa sasa kwani ndani ya wiki hii barua hiyo itakwenda FIFA kutafuta haki yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles