WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Yanga leo watakuwa kibaruani kuwakabili Cercle de Joachim ya Mauritius, kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga inayonolewa na kocha Hans van de Pluijm, itaingia uwanjani huku ikiwa na akiba ya bao 1-0 walilolipata kwenye mchezo wa awali nchini Mauritius.
Wapinzani wao timu ya Cercle de Joachim waliwasili juzi jijini Dar es Salaam wakiwa na msafara wa watu 21 tayari kwa mchezo huo.
Mara baada ya kuwasili nchini kocha mkuu wa timu hiyo, Abdel ben Kacem, alisema wamekuja nchini kuhakikisha wanapata ushindi na sio kukamilisha ratiba.
“Kikosi changu hakijaja kukamilisha ratiba ila kuja kushindana na kuhakikisha tunasonga mbele, licha ya kuwa tupo ugenini lakini nina imani tutafanya kazi ile iliyotuleta,” alisema.
Kwa upande wake kocha wa Yanga, Hans Van de Pluijm, ameshaweka wazi kuwa kikosi chake kitaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa kwani licha ya kutaka ushindi lakini inahitaji kujihami zaidi ili kutoruhusu bao langoni mwao.
“Nahitaji kushinda katika mechi yetu ya leo, lakini nimeshagawa majukumu kuhakikisha wachezaji wangu hawaruhusu bao lolote kuingia nyavuni,” alisema.
Yanga wanaingia uwanjani huku wakimkosa mshambuliaji wao, Donald Ngoma, aliyelazimika kuondoka nchini juzi na kurudi kwao baada ya kufiwa na mdogo wake huku viungo, Salum Telela na Haruna Niyonzima nao ni majeruhi.
Katika mchezo huo Yanga inahitaji ushindi wa idadi yoyote ya mabao na wakifanikiwa kuvuka hatua hiyo watakutana na mshindi kati ya APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland na kama ikivuka tena hatua hiyo, watakutana na Al Ahly ya Misri au mshindi kati ya Recreativo de Libolo ya Angola na Racing Micomiseng ya Equatorial Guinea.