26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga isijidanganye, ikaze buti

jerry muroNA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WAWAKILISHI pekee Afrika Mashariki kwenye michuano ya kimataifa, timu ya Yanga, baada ya kumaliza majukumu katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA, wanaelekeza nguvu zao katika michuano ya Kombe la Shirikisho, ambapo wamepangwa Kundi A hatua ya nane bora.

Yanga ipo kundi moja na timu za MO Bejaia ya Algeria, Madeama ya Ghana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo kipute cha kusaka nafasi ya kucheza nusu fainali kinatarajiwa kuanza Juni 17 mwaka huu.

Ukiliangalia kundi hilo kwa haraka haraka unaweza kuliona ni rahisi kutokana na viwango vya timu hizo katika ligi zao za nyumbani tofauti na Yanga ambayo imefanikiwa kuweka kibindoni makombe mawili msimu huu.

Wanajangwani wamechukua ubingwa wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 73 katika michezo 30 ya ligi ikishinda 22, kutoa sare saba na kufungwa mchezo mmoja tu huku ikiruhusu mabao 20.

Wakati timu hiyo ikiwa na uwiano huo, wapinzani wao kutoka Algeria MO Bejaia kwenye msimamo wao wa Ligi Kuu ya Algeria wanashika nafasi ya tano na pointi 43 katika ligi yenye timu 16 ambayo bado inaendelea.

Timu ambayo inaonekana kuwa tishio kwa Yanga ni TP Mazembe ambapo kwenye msimamo wa Ligi ya Kongo, inashika nafasi ya nne kati ya timu nane japo ligi bado inaendelea.

Timu ya Medeama ya Ghana ambayo inaonekana kuwa ndiyo timu dhaifu katika kundi hilo, ipo nafasi ya 11 katika ligi inayoshirikisha timu 16.

Ikumbukwe hii pekee haitoshi kupima ubora wa timu hizo, maana kwa kufanya hivyo itawapoteza kabisa Yanga katika mbio zao za kusaka ubingwa wa kombe hilo.

Akizungumzia hatua hiyo ya makundi baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kupanga makundi ya hatua waliyofikia, kocha mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, alieleza kuwa hawaihofii timu hata moja katika kundi lao.

“Tunaelekeza nguvu zetu kwenye michuano iliyopo mbele yetu, hatuzihofii timu tulizopangwa nazo kwani tunaamini tutavuka hatua hiyo ya makundi,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi.

Yanga isije ikabweteka kutokana na mafanikio yake iliyopata na kujiona bora kuliko timu nyingine katika kundi lake, ijikite katika maandalizi ya kina lengo likiwa ni kufika mbali na kuiletea sifa Tanzania.

Kitendo cha kubweteka kinaweza kuwapoteza maana ya safari ndefu iliyoanza timu hiyo na kujikuta ikiendelea kuhesabu msimu mwingine bila ya kombe la kimataifa.

Timu hiyo imetangaza kuingia kambini mara moja kujiandaa na michezo hiyo ya kundi lake, ambapo mchezo wa kwanza wataanzia ugenini.

Kambi hiyo imepangwa kuwa nje ya Mkoa wa Dar es Salaam, kwa kuwa Algeria ni nchi yenye baridi hivyo wataenda kuweka kambi sehemu itakayoendana na mazingira ya wenyeji wao.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Yanga, Jerry Muro, beki mpya wa timu hiyo Hassan Ramadhani Kessy, ataungana na kikosi hicho tayari kwa maandalizi ya mchezo huo.

“Tunategemea kuanza mazoezi na Kessy, lakini pia tumepanga kufanya usajili mdogo yote yakiwa ni maandalizi ya kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo yetu yote ijayo,” alisema Muro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles