TIMU ya Yanga leo watakuwa kibaruani kuikabili timu ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa raundi ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika utakaochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga imepata nafasi hiyo baada ya kuwatoa APR kutoka Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2 huku Al Ahly ikifanya hivyo kwa CRD Libolo ya Angola kufuatia ushindi wa mabao 2-0.
Itakumbukwa kuwa Al Ahly iliitoa Yanga mwaka juzi katika raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya timu hizo kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani na kupigiana penalti na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutupwa nje kwa penalti 4-3.
Mbali na hilo, miaka iliyopita timu hizo zilipopambana kwa mara ya kwanza vikosi vyao havikuwa na wachezaji waliopo sasa wala mabenchi ya ufundi hayakuongozwa na makocha waliopo.
Licha ya kuonekana kuna na mabadiliko makubwa katika vikosi vyote viwili hivi sasa, mchezo huo unaonekana kubeba taswira moja baina ya makocha hao ambao wote ni raia wa Uholanzi.
Historia inaonyesha kuwa mwaka 1982 timu hizo zilipokutana kwa mara ya kwanza, Yanga walikuwa wakifundishwa na kocha Geoffrey ‘Jeff’ Hudson wa Uingereza na safari hii inanolewa na Mholanzi, Hans van der Pluijm, wakati Al Ahly ilikuwa inanolewa na Mahmoud El-Gohary na sasa mikoba imeshikwa na Mholanzi, Maarten Cornelis ‘Martin’ Jol.
Van der Pluijm (67) katika maisha yake ya uchezaji akiwa beki king’ang’anizi alipata kuichezea klabu moja tu bila kuhama, FC Den Bosch ya Uholanzi kuanzia mwaka 1967 hadi 1986 alipotundika daluga na akaifundisha pia klabu hiyo kuanzia 1990-1995.
Kabla ya kutua Yanga Januari 2014, akitokea klabu ya Medeama SC ya Ghana, lakini ni huko ambako alifundisha klabu nyingi zaidi kama Berekum Chelsea, Hearts of Lions na Ashanti Gold.
Kwa upande wa Martin Jol (60) ambaye enzi zake aliwahi kucheza katika ligi mbalimbali nchini Uholanzi, Ujerumani na Uingereza, ni mmoja kati ya makocha wazoefu barani Ulaya na amezifundisha klabu za Roda JC, RKC Waalwijk na AFC Ajax za Uholanzi, Hamburger SV ya Ujerumani na klabu za Tottenham na Fulham za Uingereza.
Kutokana na historia zao kila mdau wa soka barani Afrika anasubiri kuona nani ataibuka shujaa mbele ya mwenzake katika hatua hiyo ngumu kwa kila timu zinazofundishwa na makocha wanaotoka nchi moja.
Pluijm anaonekana kutaka kurudia rekodi yake ya mwaka 2014 kwa kuibuka na ushindi nyumbani ili kutengeneza mazingira mazuri zaidi ya kusonga mbele kwenye mchezo wa marudiano.
Mara ya mwisho kwa Yanga kukutana uso kwa macho na Al Ahly ilikuwa mwaka 2014 katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam Machi mosi, Yanga ilishinda bao 1-0 lililopachikwa na nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika dakika ya 82, hii ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kuifunga timu hiyo kutoka Misri.
Hata hivyo, ziliporudiana mjini Alexandria Machi 9, Yanga ikafungwa bao 1-0 hali iliyolazimu zipigiane penalti ambapo Yanga ikatolewa kwa mabao 4-3.
Said Bahanuzi na Mbuyu Twite ndio waliokosa penalti kwa Yanga na Al Ahly ilikuwa haina haja ya kumalizia penalti yake ya mwisho.
Kwa hivi sasa Yanga inaonekana kusaka nafasi ya kucheza kwa mara ya nne robo fainali na mara ya pili hatua ya makundi ya michuano hiyo tangu iliposhiriki mwaka 1998, kwa upande wa Al Ahly wao wanausaka ubingwa wao wa tisa na kuzidi kujikita kileleni mwa timu bora za Afrika.
Katika mechi 14 zilizopita dhidi ya Misri ambazo ni Al Ahly, Ismaily na Zamalek, Yanga imeshinda mechi moja tu, imetoka sare tano na kufungwa mechi nane huku ikifunga mabao 8 na kupachikwa mabao 29.
Lakini kwa upande wa mechi dhidi ya Al Ahly, Yanga imecheza mara nane, ikishinda moja, kutoka sare mara mbili tu, zote nyumbani na kupoteza mechi tano kati ya mechi hizo nane imefungwa mabao 19-5.
Rekodi za Yanga dhidi ya Al Ahly zinaonyesha kwamba, kwa mara ya kwanza timu hizo zilikutana mwaka 1982 kwenye Klabu Bingwa Afrika.
Baada ya Yanga kuitoa Textil Pungue ya Msumbiji katika raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 4-1 (ikishinda mabao 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani), ikakabiliana na Al Ahly ambapo ilikubali kipigo cha mabao 5-0 mjini Cairo na ziliporudiana mjini Dar es Salaam ikatoka sare ya 1-1.
Mwaka huo huo Al Ahly iliendelea hadi kutwaa ubingwa huo ambapo kwenye robo fainali iliitoa Green Buffaloes ya Zambia kwa mabao 3-2, katika nusu fainali ikaifungashia virago Enugu Rangers ya Nigeria kwa jumla ya mabao 4-1 na kwenye fainali ikaitandika Asante Kotoko jumla ya mabao 4-1 pia.
Mwaka 1988, Yanga ikakumbana na Al Ahly katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika, ambapo zilitoka suluhu mjini Dar es Salaam na ikafungwa mabao 4-0 Cairo.
Al Ahly ikaendelea kuifunga Nakivubo Villa SC ya Uganda kwenye raundi ya pili jumla ya mabao 6-3, kwenye robo fainali ikaitoa Matchedje ya Maputo Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 kabla ya kuutema ubingwa wake kwa Entente Setif ya Algeria kwa mikwaju ya penalti 4-2. Kwanza ilifungwa mabao 2-0 mjini Algiers, lakini ikapata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani.
Mwaka 2009 Yanga ilipangwa na Al Ahly katika raundi ya kwanza ambapo ilifungwa jumla ya mabao 4-0. Ilifungwa ugenini 3-0 na ikafungwa 1-0 nyumbani.
Lakini ulikuwa mwaka mbaya kwa Al Ahly kwani ilitolewa na Kano Pillars ya Nigeria kwa sheria ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 3-3. Zilitoka sare ya bao 1-1 mjini Kano, ziliporudiana zikafungana mabao 2-2.
Katika raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho ambako iliingia baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa, Al Ahly pia ikatolewa kwa penalti 6-5 na Santos FC ya Angola. Kwanza ilishinda 3-0, halafu ikafungwa 3-0 mjini Luanda.
Ukiacha kiwewe cha kutofanya vizuri kwenye mechi za kimataifa, Yanga kwa ujumla imekuwa na mkosi mbele ya timu kutoka Afrika ya Kaskazini.