31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

YALIYOJIRI MZUNGUKO WA KWANZA LIGI KUU BARA

Na MARTIN MAZUGWA

LIGI Kuu ya Tanzania Bara mzunguko wa kwanza unafika tamati wikiendi hii kwa timu zote zinazoshiriki kushuka viwanjani kumaliza michezo 15 kwa kila moja.

Simba bado ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 32 mara baada ya kushuka uwanjani mara 14 ikifuatiwa na Azam FC ‘Wanalamba lamba’ ambao wamejikusanyia pointi 30 katika michezo14.

Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’ wanamaliza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Majimaji ya Songea wakati Azam FC wakimaliza na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga wanaoshika nafasi ya tatu katika msimamo huo.

Mchezo wa Azam pamoja na Yanga unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na ushindani uliopo, ambapo Azam watakuwa wakitaka kushinda ili wakae kileleni huku Wanajangwani wakihitaji kupunguza idadi ya pointi kwa mahasimu wao.

Haya ni baadhi ya matukio ambayo yamejitokeza katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambao unaenda kumalizika kesho.

Singida United yawaacha wadau vinywa wazi

Moja kati ya timu zilizowaacha vinywa wazi mashabiki na wadau wa soka nchini Tanzania msimu huu, ni Singida United ambao wamepanda daraja msimu huu ambao wamekuwa katika kiwango bora zaidi na kushika nafasi ya tano wakiwa na pointi 24 na  kufuata nyayo za Mbeya City, ambao katika msimu wa kwanza 2013-14 walikamata nafasi ya tatu katika mzunguko wa kwanza wakiwa na pointi 27.

Kiyombo aliyezitungua Simba, Yanga

Kati ya washambuliaji waliokuwa katika kiwango bora msimu huu ni Habibu Kiyombo wa Mbao FC, ambaye hadi sasa amepachika mabao saba sawa na Mohamed Rashid wa Tanzania Prisons.

Kiyombo ndiye mshambuliaji pekee ambaye amezifunga timu kongwe za Simba na Yanga, alianza kuwatungua Wekundu wa Msimbazi katika mchezo uliopigwa Septemba 21 mwaka     uliopita ulioisha kwa sare ya mabao 2-2 kisha akamalizia na Yanga kwa kuwafunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0.

Mbeya City, Ruvu Shooting nyanya

Hadi sasa ni timu mbili pekee, Ruvu Shooting pamoja na Mbeya City ‘Wagonga Nyundo’  zimefungwa mabao mengi zaidi  kuliko timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara katika  mzunguko huu, ambapo kila moja imeruhusu wavu wake kuguswa mara 19 na hivyo safu zao za ulinzi kuonekana nyanya, huku maafande hao wakikamata mkia katika msimamo.

Sajili zilizolipa msimu huu

Msimu huu umekuwa wa neema kwa baadhi ya wachezaji waliohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, ambapo baadhi ya wachezaji wameanza kulipa fadhila kwa klabu zao mpya, Ibrahim Ajib kutoka Simba kwenda Yanga tayari amefunga  mabao matano, Mohamed Rashid kutoka Kijichi FC kwenda Prisons mabao saba.

Wengine ni raia wa Uganda, Emmanuel Okwi, aliyejiunga na Simba akitokea SC Villa  mabao 11 akiwa ndio kinara wa ufungaji naye John Bocco ambaye ametoka Azam kwenda  Simba amepachika mabao matano.

‘Mapro’ waliong’ara mzunguko huu

Timu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara misimu ya hivi karibuni zimekuwa zikisajili wachezaji wa kigeni kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao, hadi sasa ni klabu mbili zimelamba dume ambapo ni Simba na Singida United, ambapo Wekundu wa Msimbazi nyota wake wawili Emmanuel Okwi na Asante Kwasi, kwa pamoja wameweka kimiani mabao 16 huku Singida United, Dany Usengimana, akipachika mabao 3.

Okwi raia wa Uganda ndiye kinara wa ufungaji akiwa na mabao 10 huku Kwasi akishika nafasi ya tatu na mabao sita.

Timu zilizovuna pointi nyingi ugenini

Vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara licha ya kuongoza katika msimamo, lakini pia ndio timu iliyokusanya pointi nyingi zaidi ugenini ikikusanya pointi 10 ikifuatiwa na mtani wake wa jadi Yanga iliyokusanya pointi tisa sawa na Azam FC wanaoshika nafasi ya pili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles