MALABO, GUINEA IKWETA
ALIYEKUWA Rais wa Gambia, Yahya Jammeh amewasili nchini Guinea ya Ikweta, siku moja baada ya kuachia ngazi kumpisha Rais Adama Barrow, aliyeshinda katika uchaguzi wa rais uliofanyika Desemba mwaka jana.
Jammeh alisafiri kwa ndege kutoka Banjul hadi Guinea kabla ya kuendelea na safari yake hadi hapa.
Hatua yake hiyo imekuja baada ya kiongozi huyo aliyetawala Gambia kwa mkono wa chuma kwa miaka 22 kukubali kuachia ngazi.
Aliachia ngazi baada ya Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kumshututisha kufanya hivyo ikitishia kumuondoa kwa nguvu iwapo angeendelea kukaidi.
Jumuiya hiyo inasema imesitisha oparesheni yake ya kijeshi Gambia lakini wanajeshi elfu saba watasalia nchini humo kudumisha usalama, huku Adama Barrow aliyeapishwa nchini Senegal akitarajiwa kurejea nyumbani muda mfupi ujao.
Kwa mujibu wa Rais wa ECOWAS, Marcel Alain de Souza, hakuna hatua zozote za kisheria zitakazochukuliwa zinazoweza kuvunja utu wake, usalama na hadhi ama familia yake.
Hiyo ni kwa mujibu wa makubaliano kupitia azimio lililofikiwa na Umoja wa Afrika (AU na Umoja wa Mataifa (UN).
Taarifa hiyo imesema Jammeh anaweza kurejea Gambia wakati wowote na mali zake hazitazuiliwa.
Kuondoka kwa Jammeh kunamaliza mzozo wa kisiasa baina yake na Adama Barrow.
Mkuu wa majeshi, Osman Badjie, amesema jeshi lake litaendelea kumtii kiongozi aliye madarakani, na kusaidia hatua za kuwarejesha raia waliokimbia hofu ya machafuko.