Na LAWRANCE MALEMBEKA-DAR ES SALAAM
BAADA ya kumalizika mkutano wa Jukwaa la Uchumi (World Economic Forum) uliofanyika mwaka huu kule Davos, Uswisi, kulikuwa na taarifa nyingi mojawapo ikiwa ni kumalizwa kwa mgogoro baina ya Serikali ya Uganda na Kampuni ya simu ya MTN.
Taarifa hizo zilitolewa baada ya mkutano uliofanyika huko Davos kati ya Ofisa Mtendaji Mkuu wake na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni. Ikulu ya Uganda ndiyo iliyotoa taarifa kwamba mgogoro kuhusu leseni ya MTN kuendelea na shughuli zake nchini humo umemalizwa na mkutano huo.
Hata hivyo, kwa wafuatiliaji wa masuala ya mawasiliano na siasa za nchi ya Uganda, taarifa za karibuni zinaonyesha kwamba mgogoro huo haujamalizika kama ambavyo ilidhaniwa huko nyuma.
Wiki iliyopita tu, mamlaka za Uganda zilitoa madai kwamba MTN imekuwa ikitangaza kupata faida kidogo ya kiwango halisi na hivyo imekuwa ikilipa kodi kidogo kuliko inavyotakiwa.
Kwa upande wake, MTN inadai kwamba uhakiki wa mapato na matumizi yake umefanywa na taasisi za kimataifa na kwamba mara zote imekuwa ikilipa kodi inayostahiki.
Wakati mgogoro huo mpya ukianza kufukuta, Serikali ya Uganda ilitangaza kumfukuza nchini humo aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa MTN Uganda, Wim Vanhelleput.
Hadi wakati naandika makala haya, Serikali ya Uganda imekuwa ikitoa kauli tofauti kuhusu nini hasa kimesababisha ichukue uamuzi huo mzito dhidi ya mabosi hao wa MTN.
Taarifa za awali za Serikali zilikuwa zikiwatuhumu mabosi hao wa MTN kwa kufanya mambo yanayohatarisha usalama wa taifa la Uganda, lakini katika siku za karibuni imekuwa ikidai kwamba watu hao wametendewa hivyo kwa sababu ya kuisababishia Serikali hasara.
Kwa vyovyote vile iwavyo, taarifa hizi kutoka Uganda zinatoa picha kwamba sakata hili la MTN na Serikali halijaisha bado na huenda kuna mengine makubwa yanafuata baada ya haya yanayoendelea.
Pasipo shaka yoyote, mgogoro huo wa MTN na Serikali ya Uganda umeanza kuathiri mapato ya kampuni hiyo na bila shaka kunaweza kukawa na athari katika ukusanyaji wa kodi huko mbele ya safari.
Uganda ni jirani zetu. Tunatakiwa kulifuatilia suala hili kwa makini kiasi kwamba kama yatatokea matatizo ya namna hii hapa kwetu, tuwe na namna ya kuyashughulikia vizuri kuliko wanavyofanya jirani zetu.
Wahenga wametuachia msemo mmoja muhimu sana; tujifunze kutokana na makosa ya wenzetu.
Hasa katika kipindi hiki ambacho kampuni zinatumia fursa za kuwekeza kwa nguvu katika eneo la mitandao ili kufanikisha maendeleo kupitia matumizi ya teknolojia.
Pia kwa wafuatiliaji wa masuala ya sekta hii ya teknolojia na mawasiliano, mtakubaliana na hoja kwamba ni umuhimu kwa sasa kwa kampuni za mawasiliano kuunganisha nguvu; kwamba kwa kufanya hivyo maendeleo yanachochewa.
Kwa sababu teknolojia mpya zinazotarajiwa kuibuliwa katika siku za usoni bila shaka zitakuja kwa gharama kubwa.
Sasa ili kushawishi wamiliki wa kampuni hizi kuongeza uwekezaji mkubwa wa namna hii, ni lazima kuwe na vivutio vya kuwafanya wafanye hivyo.
Na kivutio kikubwa kuliko vyote cha kuwafanya wawekezaji waone faida ya kuwekeza ni kuwaonyesha kwamba kwa kufanya hivyo watapata faida. Faida ndiyo kiu hasa ya wafanyabiashara na wawekezaji.
Hata hivyo, ukweli ulio dhahiri unaonyesha kwamba kama kutakuwa na washindani wengi wanaoshindana katika sekta hii, ni vigumu kwa kampuni moja kufanya uwekezaji mkubwa peke yake.
Hii ni kwa sababu wamiliki wanajua kwamba ushindani huo unamaanisha uwezekano wa kupata faida ni mdogo kulinganisha na uwekezaji uliofanyika.
Kwa hiyo muunganiko wa kampuni za simu unatakiwa kutoa mwangwi kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki (ikiwamo Tanzania) kuhusu umuhimu wa kampuni za mawasiliano kuunganisha nguvu kwa ajili ya maendeleo ya haraka ya nchi zetu hizi.
Bila shaka, Tanzania kwa sababu ya ukubwa wa eneo lake na idadi kubwa ya watu wake, itafaidika zaidi na uunganishaji nguvu wa kampuni za mawasiliano zinazofanya kazi zake hapa nchini.
Wenzetu wameanza kuliona hili mapema. Twende kwa kasi zaidi.