Derick Milton, Maswa
Katika kupambana na changamoto zinazowakumba watoto wa kike mashuleni pindi wanapokuwa kwenye hedhi, Shirika la World Vison Tanzania limezindua kampeni inayolenga kutatua changamoto hizo.
Kampeni hiyo iliypewa jina la ‘Hedhi Salama kwa Watoto wa Kike’ imezinduliwa jana katika kijiji cha Shishiyu wilayani Maswa mkoa Simiyu, ambapo imeendana na maadhimisho ya siku ya hedhi salama duniani.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Meneja wa shirika hilo Kanda ya Nzenga yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Tabora John Massenza, amesema kampeni hiyo itahusisha ujenzi wa miundombinu ya maji na na vyoo vyenye mahitaji maalumu mashuleni.
“Katika kampeni hiyo, World Vision itatoa mafunzo ya hedhi salama kwa walimu, wanafunzi viongozi wa vijiji na kata, ili kutengeneza mazingira rafiki kwa wasichana wakiwa kwenye hedhi.
“Takwimu zinaonyesha kuwa kila mwezi watoto wengi wa kike nchini wanakosa masomo kwa siku tatu hadi tano na kwa mwaka siku 30 hadi 60 wanakosa masomo hali ambayo inayowafanya kutofanya vizuri darasani,” amesema.
Massenza amesema kipindi cha hedhi kimekuwa ni kipindi kigumu sana kwa watoto wa kike hasa wa vijijini, World Vision ikaona kutoa elimu tu haitoshi bali kutengeneza mazingira rafiki yatakayomsitiri msichana akiwa katika hedhi ni muhimu kwa utu na maendeleo ya msichana.