Damian Masyenene – Kahama
HALMAShAURI ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, imeikabidhi Wizara ya Viwanda na Biashara ekari 62 ambazo zimetolewa bila malipo eneo la uwekezaji (EPZA) Nyashimbi kwa ajili ya ujenzi wa kituo maalumu cha utafiti wa mazao hususan ya pamba na maendeleo.
Eneo hilo ambalo ni sehemu ya kitakapojengwa kituo cha uwekezaji wa kiuchumi (Special Economic Zone) ambacho kitamilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Kahama, wizara italitumia kwa ajili ya kuendeleza teknolojia ya uchakataji pamba na utengenezaji wa mafuta yake pamoja na viwanda vingine.
Hayo yalisemwa mjini Kahama juzi, wakati wa ziara ya siku moja ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe ambaye alitembelea pia Kiwanda kipya cha KOM Food Products Co. Ltd kinachojengwa eneo la Chapulwa ambacho kitajihusisha na utengenezaji wa vinywaji maji, soda na juisi) na vifungashio ili kuyapa thamani mazao ya chakula na mifugo kikiwa kimegharimu Dola za Marekani milioni 10, ambapo kitakuwa na uwezo wa kutoa ajira za kudumu 200 na za muda 2,000.
Profesa Shemdoe ambaye aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji, alitembelea pia eneo la wajasiriamali na viwanda vidogo la Zongomela mjini hapa linalojumuisha wajasiriamali 1,545 lenye ukubwa wa ekari 500 wanaofanya shughuli za uselemala, wauzaji wa mbao, madirisha, vitanda na bidhaa za chuma.
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake, Profesa Shemdoe, alisema sasa Tanzania inavyo viwanda 8,447 vyenye ukubwa mbalimbali, ambapo alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kusogeza huduma katika kiwanda cha KOM Food Products ili uzalishaji uanze kwa wakati, huku pia akiagiza SIDO kuweka mazingira rahisi ya wajasiriamali wadogo kupata mikopo.
“Kuna makubaliano yamefanyika kati ya SIDO, VETA, Benki ya Azania na NSSF pamoja na wizara kwa ajili ya kuweka mazingira salama kwa wajasiriamali na wawekezaji wadogo kwahiyo SIDO kupitia mfuko wa NEDIA mtengeneze mazingira wajasiriamali wapate mkopo huo.
“Tutawasemea (wajasiriamali wadogo) na tutapendekeza hizi Fenicha za ndani zianze kutumika kwenye ofisi za Serikali kwa sababu zina ubora wa hali ya juu na naomba hili lianze wilayani na ofisi za mkoa kuwaunga mkono wajasiriamali wadogo,” alisema Prof. Shemdoe.
Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi Profesa Mpanduji alisema sasa wanatoa mikopo ya Sh milioni 5 kwa wajasiriamali, lakini kutokana na mpango wa ushirikiano walioingia na benki ya Azania utawawezesha kutoa mikopo ya kuanzia Sh milioni 8 hadi 500, ambapo eneo la Zongomela limetengewa Sh milioni 140.5 kwa ajili ya wajasiriamali hao kukopa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema eneo hilo lenye wafanyabiashara 1,545, likiwa na ukubwa wa ekari 500 limechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya viwandani mkoani hapa na kufikia 729, linakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara ambapo mwaka huu wamejiandaa kutengeneza barabara yenye urefu wa Km 14.5 kwa kiwango cha lami ndani ya eneo hilo la kibiashara.
Katibu wa eneo la viwanda vidogo la Zongomela, Jerad Egwasa alisema taasisi za kifedha zinapaswa kuwatambua na kuwapa thamani lakini pia serikali kupitia taasisi zake kufanya malipo kwa wakati wanapoagiza bidhaa kutoka kwao, huku mwenyekiti wa mafundi Selemala, Shaban Nkindiko akiomba eneo hilo kusaidiwa wataalam na ofisi ya maliasili ili kurahisisha elimu na huduma za mazao ya misitu.