29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara ya Elimu yaanika mikakati yakuboresha sekta hiyo

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ametaja mikakati mitatu ya kuboresha sekta ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuandaa mitaala ambayo itaendana na sera ya ualimu ambapo amedai ubora wa elimu ni pamoja na kuwa na walimu na wakufunzi wakutosha na wenye ubora.

Mikakati mingine ni kuandaa walimu na wakufunzi wa kutosha lengo likiwa ni kuongeza ubora wa elimu ,pamoja na kuwa na miundombinu rafiki kwa wanafunzi na walimu.

Prof. Mkenda ameelezwa hayo Februari 21,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza katika hafla ya ugawaji wa kompyuta 300 zinazotokana na mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) kwa vyuo vya ualimu 13.

Vyuo vya vilivyopatiwa Kompyuta ni pamoja na Marangu, Kleruu, Vikindu, Patandi, Korogwe, Mpwapwa, Shinyanga, Ilonga, Tarime, Tandala, Butimba, Mtwara na Morogoro.

Waziri Mkenda amesema kwa sasa ni lazima wapitie mitaala kwa kupitia sera ambapo amedai suala la ubora wa elimu ni pamoja na kuwa na walimu na wakufunzi wa kutosha.

“Jambo la kwanza ni mitaala lazima iwe zao la sera,sera tunayo lakini tunaipitia upya na hili tutalifanya haraka na maana yake mitaala itabadilika tunaanza utekelezaji mara moja tutaanza taratibu kuhakikisha linafika. Hili suala litakuwa shirikishi na tutakuwa na mkutano mkubwa kushirikisha wadau.

“Pili ni kuandaa walimu na wakufunzi kuongozea ubora wa elimu na tatu ni miundombinu na vitendea kazi vya walimu ikiwa ni pamoja na vitabu vya kiada na ziada kuwa na Maktaba  iliyosheheni vitabu na ni kweli kwenye ofisi yangu pale nimewambia waniletee vitabu vyote vinavyotumika kufundishia vyote kuanzia Pre-School.

“Lazima tupitie mitaala kwa kupitia sera, suala la ubora wa elimu sio peke yake suala la kuwa na walimu na wakufunzi ni suala muhimu unaweza ukawa na mitaala mizuri lakini walimu hawatoshi hata wanafunzi wanaosoma shule za binafsi na Serikali performance yao inatofautiana,” amesema Prof. Mkendana kuongeza kuwa:

“Suala la mitaala na kuwaandaa walimu wa kutosha katika hilo tutafanya kazi na Tamisemi kuhakikisha tunakuwa na walimu wa kutosha pamoja na kuwagawa kwa haki kwa sababu mijini kuna walimu wengi,”amesema.

Waziri Mkenda amesema Wizara inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Vyuo mbalimbali nchini ikiwemo ukamilishaji wa Chuo cha Kabanga,ambapo amedai ujenzi  wa vyuo vipya vya Sumbawanga, Dakawa, Mhonda na Ngorongoro ujenzi unaendelea.

Aidha amesema ukarabati na ujenzi wa baadhi ya miundombinu katika vyuo vya Morogoro, Mpwapwa, Tukuyu, Kasulu, Butimba na Patandi nao unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwaka huu wa fedha 2021/2022.

“Hadi sasa Wizara imetoa mafunzo ya matumizi ya Tehama katika kufundishia na kujifunzia kwa wakufunzi wote 2,300 kutoka Vyuo vya Ualimu vya Serikali yote 35,”amesema.

Awali,Naibu Waziri wa Elimu, Omari Kipanga amesema bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa walimu nchini hivyo kunahitajika jitihada ili kuzaliwa walimu wengine wengi kupitia vyuo hivyo.

“Kila mwaka ni lazima tuzalishe walimu wa kutosha,Serikali ni kweli imewekeza ila bado kuna changamoto ya walimu bila walimu hatuwezi kutoka nyinyi ni chemchem ila tunaenda kubadilisha mitaala tutaangalia haya masuala ya teknolojia,”amesema Kipanga.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Prof. Caroline Nombo amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Canada ambapo amedai mchango wa Canada katika mradi huo ni jumla ya Dola za Canada milioni 53.

Amesema mchango wa Serikali ya Tanzania ni katika kugharamia shughuli mbalimbali za uendeshaji wa vyuo ikiwemo gharama za malipo ya chakula kwa wanachuo na mafunzo ya ualimu kwa vitendo.

Kaimu Katibu Mkuu huyo amesema dhumuni kuu la mradi huo ni kuendeleza elimu ya ualimu,kwa kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji kupitia uboreshaji wa miundombinu ya utoaji wa mafunzo ya ualimu katika vyuo vya ualimu vya Serikali 35.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles