Na Clara Matimo, Mwanza
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,imetaja vipaumbele vyake ikiwemo ni pamoja na kuanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi (Land Governance Framework) ili kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika kutoa huduma za sekta hiyo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Angeline Mabula, alibainisha hayo juzi jijini Mwanza, wakati akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya wizara yake katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa waandishi wa habari.
Alisema katika kuimarisha mifumo ya utawala bora, uwajibikaji na kudhibiti ukiukwaji wa maadili kwa watumishi wa sekta ya ardhi, wizara hiyo imeanzisha mfumo utakaongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi.
Akieleza jinsi watakavyotatua na kudhibiti migogoro ya ardhi alisema
wizara imejipanga kubadilisha nyaraka za upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi kutoka analogia kuwa za kidigitali kama mpango wa muda mrefu, uwepo wa madawati ya kushughulikia malalamiko katika ofisi za ardhi za mikoa, kutoa elimu kwa umma wakishirikiana na wadau mbalimbali.
Aidha ameeleza kwamba wataongeza kasi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, wataweka rejista ya migogoro ya ardhi kwa kila ofisi za ardhi za mikoa na halmashauri zitakazoonesha aina na hali ya mgogoro pamoja na namna ilivyoshughulikiwa, mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya mapya 59 kuanza kutoa huduma na hivyo kuwa nayo katika wilaya zote nchini, kukamilisha ujenzi wa mfumo wa kusimamia mashauri katika mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya na kuanza kutumika.
“Lengo ni kurahisisha utendaji kazi wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika kutunza kumbukumbu za mashauri, kufungua mashauri mapya, kufuatilia utendaji kazi wa watumishi wa mabaraza hayo na upatikanaji wa nakala za hukumu kwa njia ya mtandao,”alifafanua Dk. Mabula.
Alisema katika mwaka wa fedha 2022/23, wizara yake inatarajia kukusanya Sh bilioni 250.1 kutokana na maduhuli ya Sekta ya Ardhi kwa kutekeleza mikakati hiyo ambayo imeainishwa katika hotuba ya bajeti.
Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni usalama wa miliki za ardhi ambapo alifafanua kwamba
kupitia mradi wa uboreshaji wa Milki za ardhi ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2027/28 kwa mkopo wa riba nafuu USD milioni 150 watajenga ofisi za ardhi katika mikoa 25 zitakazokidhi utoaji huduma kwa mfumo unganishi wa kuhifadhi taarifa za ardhi (ILMIS).
Pia huduma zote za sekta zitakuwa zikitolewa katika majengo hayo zikiwemo Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya, kujenga ofisi za ardhi za mikoa, kuboresha mfumo wa ILMIS, kutoa hati miliki 150,000 katika halmashauri 10 nchini za kimila 50,000 katika Vijiji 50, kuanda mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 50 katika wilaya sita, kutoa leseni za makazi 250,000, kuimarisha miundombinu ya upimaji na ramani kupitia mradi wa uimarishaji wa miundombinu ya Upimaji na Ramani(NSDI) utakaotekelezwa kwa fedha za mkopo wa riba nafuu wa USD milioni 65 kupitia Benki ya Exim.
“Kwa upande wa urasimishaji makazi wizara itashirikiana na Mamlaka za Upangaji na sekta binafsi ikiwa ni hatua ya kukamilisha Programu ya kurasimisha makazi na kuzuia makazi yasiyopangwa mijini ambayo ilianza mwaka 2013 itaisha mwaka 2023 baada ya muda huo wizara itafanya tathmini ya mafanikio na changamoto ya utekelezaji wa programu hii.
“Hivyo wizara inaendelea kuwasisitiza wananchi wote wanaoishi katika maeneo ambayo hayajapangwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika zoezi la urasimishaji ikiwemo kuchangia gharama za urasimishaji na gharama za hati ili waweze kurasimishiwa maeneo yao na kupata haki miliki za viwanja vyao,” alifafanua Dk. Mabula.