29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara ya Ardhi kutoa hati za ardhi kwa siku moja Sabasaba

Na Munir Shemweta, WANMM

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itatoa hatimiliki za ardhi ndani ya siku moja kwa wananchi waliokamilisha taratibu za kupatiwa hati kwenye zoezi la urasimishaji makazi holela katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wakati wa Maonesho ya 45 Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ardhi, Lusajo Mawakabuku Juni 27, 2021 wakati akielezea mipango na mikakati ya Wizara yake katika ushiriki wa maonesho ya Sabasaba yanayofanyika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

Amesema, kwa mwaka huu kwenye maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Wizara imejipanga vizuri kuhakikisha inatoa na kutangaza huduma zinazotolewa ili kukidhi kiu wa wananchi watakaotembelea Banda la Wizara ya Ardhi.

Kwa mujibu wa Mwakabuku, wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani watakaoweza kupata Hatimiliki za Ardhi papo hapo katika Banda la Wizara (One Stop Shop) ni wale ambao maeneo yao yamefanyiwa urasimishaji na viwanja kupimwa.

Mwakabuku amesema, nyaraka zinazotakiwa kwa mmiliki wa kiwanja anayetaka kupatiwa hati ni michoro ya mipango miji, ramani ya upimaji, fomu ya majirani, kitambulisho cha uraia pamoja na barua ya maombi.

Kupitia maonesho hayo ya Sabasaba Mwakabuku amesema, wananchi wataweza pia kununua ramani zenye wilaya mpya za Tanzania sambamba na wale wenye migogoro ya ardhi kuweza kuwasiliana moja kwa moja na makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa ili kupata ufumbuzi wa migogoro katika maeneo yao.

Pia wananchi watakotembelea Banda la Wizara ya Ardhi watapata maelezo kuhusiana na huduma za Mipango Miji, Maendeleo ya Makazi, Uthamini, Upimaji na Ramani pamoja na Huduma za Ukadiriaji na Ulipaji Kodi ya Pango la Ardhi ambapo wataweza kupatiwa ankara za malipo kwa ajili ya kwenda kulipia benki.

Mkuu huyo wa kitengo cha mawasiliano serikali Wizara ya Ardhi aliongeza kuwa, Wizara yake kwa sasa inaendelea kuboresha huduma zake ikiwemo mifumo ya utunzaji na utoaji hati za ardhi ambapo kwa sasa inatoa hati za kielektroni za kurasa moja mkoani Dar es Salaam na kutarajiwa kuanza kutoa hati za aina hiyo katika mkoa wa Dodoma mwezi Julai mwaka huu.

Aidha, alisema katika jitihada za kuondoa kero za ardhi kwa wananchi, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi iko katika hatua za mwisho za kuanzisha Kituo cha Mawasiliano (Call Center) ambapo kupitia kituo hicho wananchi wataweza kuwasilisha moja kwa moja kero za ardhi kwa njia ya simu bila kulazimika kwenda ofisi za ardhi.

Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanaanza rasmi siku ya jumatatu tarehe 28 Juni 2021 na kumalizika Julai 10, 2021 ambapo kauli mbiu ya maonesho hayo kwa mwaka huu wa 2021 ni Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles