Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, imetoa tahadhari na njia za kuepuka magonjwa ya mlipuko kutokana na kuanza kunyesha mvua kubwa katika baadhi ya maeneo, ikiwemo Mkoa wa Dar es salaam.
Pia imewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikali za mitaa, wananchi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila eneo haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya milipuko.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi alisema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, kuna uwezekano mkubwa kuibuka magonjwa ya milipuko kama kuhara damu,kipindupindu na yale yanayoenezwa na mbu ambayo ni malaria na dengue.
“Wote tumeshuhudia kuanza kujitokeza kwa uharibifu wa miundombinu ikiwemo ile ya kusafirisha na khifadhia maji safi na taka ambapo hali hii itahatarisha afya ya jamii na hivyo kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko,”alisema.
Alizitaja kanuni wanazotakiwa kufuata wananchi ni pamoja na kuchemsha maji ya kunywa,kuepuka kula chakula kilichopoa,au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama.
Alizitaja kanuni zingine ni kutumia ipasavyo vyoo na kunawa mikono kwa maji safi na tiririka na sabuni kabla ya kula,baada ya kutoka chooni,baada ya kumnawisha motto aliyejisaidia na baada ya kumhudumia mgonjwa.
Alizitaja kanuni zingine ni kuosha matunda na maji safi kabla ya kula,kuongeza usimamizi wa usafi wa jumla na mikono katika maeneo ya mikusanyiko kama shuleni,vyuoni na masokoni.
Alizitaja sababu zingine ni kutotapisha vyoo,kujikinga kuumwa na mbu pamoja na kutumia vyandarua,kusimamia hali ya usafi katika mifumo ya maji safi,maji taka na mitaro.
Aliwataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikali za mitaa wananchi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila eneo haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya milipuko.
“Kwa hiyo nawaomba sana waganga wetu wa wilaya wachukue ‘leadership’ katika hili na kuweza kushirikiana na mamlaka ndani ya eneo lao hakuwi chanzo.Wizara inaendelea kuwakumbusha tiba ni bora kuliko kinga,”alisema.