26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

WIZARA MBILI ZAWEKWA MTEGONI

Na AGATHA CHARLES 

RAIS John Magufuli amezinyooshea kidole Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na ile ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, huku akisema hajaridhishwa na utendaji wa wizara inayoshughulikia mambo ya nje.

Alisema Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa ikitoa ajira kiholela kwa maofisa wa mbalimbali balozi za Tanzania nje, kutofanya vyema diplomasia ya uchumi na madai ya watu wasio watumishi wake kuiongoza kwa ‘rimoti’.

Kwa upande wa Wizara ya Elimu, Rais ameitahadharisha juu ya ugawaji bora wa Sh bilioni ya 147 ambazo zimetolewa na Serikali kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, akisema hatarajii kuona mwanafunzi mwenye sifa ya kupata mkopo akifika chuoni azungushwe kupewa fedha hizo.

Akizungumza Ikulu, Dar es Salaam jana, baada ya kuwaapisha wakuu wapya wa mikoa, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu, Rais alisema hafurahishwi na mwenendo wa utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, hivyo ameamua kuifanyia mabadiliko kwa kumteua Profesa Adolf Mkenda atengeneze mfumo mpya unaoendana na sera ya diplomasia ya uchumi.

Alisema hafurahishwi na mwenendo wa utendaji wa wizara hiyo, hasa anaposikia kwamba kuna watu wengine wanaiendesha kwa ‘rimoti’ wakati si wafanyakazi wa hapo.

Katika maelezo yake yaliyotumia dakika 16, alisema ameona kuwa, ndani ya wizara hiyo kuna udhaifu kidogo, hivyo akaamua kumteua Profesa Mkenda,  ambaye ni mchumi mbobezi na alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda ili aende kujenga mfumo imara unaoendana na sera iliyopo.

“Mambo ya Nje niliona pana udhaifu kidogo. Tunapozungumzia uchumi wa viwanda tunazungumzia mambo yetu yaende kiuchumi uchumi, nikasema ngoja nimpeleke huyu mchumi mzuri nikaone kama kutakuwa na mabadiliko, kwa hiyo nataka aende pale akapabadilishe, si kufanya kazi ya kibalozi balozi tu,” alisema Rais.

Alisema anataka kila balozi kwenye nchi aliyopo, baada ya muda fulani aeleze ameiletea nchi wawekezaji wangapi na si kwenda kunywa mvinyo.

“Lakini ninataka pia pawe na mfumo ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje, kwa sababu pamekuwa na tabia kila anayeshindikana mahali anapelekwa hapo. Kama kuna mtumishi huko hafaifai anapelekwa kupumzika Marekani.

“Kwenye balozi zetu kule pamekuwa na over employment (wajiriwa wengi kuliko mahitaji), Ubalozi wa Brazil hapa Tanzania una watu wanne tu kwenye ofisi yao, wengine  wanawatumia wafanyakazi wa ndani. Nenda ubalozi wetu wa Ethiopia au mahali fulani utakuta wamejaa, pale Ethiopia tu madereva walioajiriwa ni zaidi ya nane.

“Sasa inawezekana haya yalikuwa yanafanyika wakati hatukuwa na uchumi wa kujua uchungu wa hela.  Nimekupeleka wewe ukaujue uchungu wa hela za Watanzania, ukafanye reforms (mabadiliko) na bahati nzuri una waziri mzuri sana, mzee Mahiga (Dk. Augustine Mahiga), ni Balozi aliyebobea. Kafanyeni mabadiliko, nchi hii ni yetu, lazima twende mbele tufanye mabadiliko kwa manufaa ya nchi yetu,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu Wizara ya Elimu, Rais alisema Septemba 29 aliidhinisha Sh bilioni 147 ili zipelekwe Wizara ya Elimu kwa ajili ya kutoa mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu.

Alisema anajua vyuo vikuu vimeanza kufunguliwa, hivyo atashangaa kama kutakuwapo wanafunzi ambao wapo kwenye orodha ya kupewa mikopo  lakini wasipewe.

“Nitashangaa sana kwa sababu nimeishaidhinisha Sh bilioni 147 na inawezekana zimeshatoka. Isije ikafika wanafunzi wamefungua, wako vyuoni wakaanza kuhangaikia mkopo na wakati wapo kwenye orodha ya kupewa. Nitajua hizo fedha zimechukuliwa  zimewekwa kwenye benki, inawezekana kwenye fixed deposited account (akaunti maalumu ya kuweka fedha kwa muda) zinamzalishia mtu fulani akachelewesha kwenda mahali fulani, huko ndiko hatutafika,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, alipongeza maelezo ya awali ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, kuwa wakuu wa mikoa ni wenyeviti wa Kamati za Maadili za Mikoa na kwamba viongozi wa mahakama watakuwa wamejua hilo.

“Nina uhakika viongozi wa mahakama walioko katika mikoa hiyo wamesikia maelezo yako (Jaji Mkuu Juma) kwamba wakatambue wenyeviti wao ndio hawa.

“Hilo mimi nimefurahi  na hawa wakuu wa mikoa wameelewa na wale wa mahakamani kule nina uhakika kutokana na maelezo yako nao watakuwa wameelewa kwamba watakapoitwa kwenye kamati za maadili hakuna atakayelalamika kwamba ameingiliwa, bali itakuwa ni kutokana na sheria na maelekezo ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu viongozi aliowaapisha, alisema: “Ninyi ni wawakilishi tu wa Watanzania milioni 55, nendeni mkawe sauti yao, mkawe wasemaji wao, kila mtakachokuwa mnakifanya mtangulizeni Mungu katika kuwahudumia watu wake. Nina uhakia mkizingatia haya yote mtaweza kujibu hoja za Watanzania ambazo ni nyingi,” alisema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli alibadili kituo cha kazi cha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Christina Mdeme kwa kumpeleka Mkoa wa Ruvuma na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk. Binilith Mahenge akamhamishia Dodoma.

“Tumempromoti Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na katika maelezo yamesema atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,  nimefanya mabadiliko, kwa sababu amekuwa promoted pale  hawezi akabaki pale, kwa hiyo atakapotoka hapa atakwenda kuripoti Ruvuma na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ndio atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,” alisema Rais.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wakuu wapya wa mikoa watambue kuwa wao si watawala, bali ni watumishi, hivyo waende wakawatumikie Watanzania, hususan masikini.

RC Mdeme

Akizungumzia mabadiliko ya ghafla ambayo yalitolewa na Rais Magufuli kwa kubadilishana na Dk. Binilith Mahenge, ambaye awali alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mdeme alisema aliyapokea vyema na kuyafurahia kwa kuwa kote anakwenda kutumikia Watanzania.

“Unapoapa ni kwamba uko tayari kufanya kazi kokote, nimepokea kwa mikono miwili na wote wanahitaji kutumikiwa,” alisema Mdeme.

Alisema anakwenda kuwatumikia watu wa Ruvuma na hivyo kuwaahidi ushirikiano ili kuhakikisha kuwa taratibu za nchi zinasimamiwa na kuleta maendeleo.

Mnyeti

Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, alisema hakuna jambo jipya wala ahadi mpya kwa mkoa huo na kwamba anakwenda kusimamia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Katiba.

Malima

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Malima, alisema atapambana kuhakikisha kuwa changamoto za mkoa huo, ikiwamo afya, kilimo, elimu, ulinzi na usalama, zinaimarika.

“Utumishi wa Mkuu wa Mkoa ni unyenyekevu kama Rais alivyosema na zaidi ni kutumikia maisha ya Watanzania. Ni kuangalia Mara kuna nini na kuboresha ili kuinua uchumi,” alisema Malima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles