JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA
AKIHESABIWA kama Mama wa Afrika Kusini ‘mpya’, taswira ya Winnie Madikizela Mandela kama mwanaharakati shujaa na shupavu mpinga ubaguzi wa rangi iliharibika wakati ilipofichuka alikuwa mwanaitikadi kali aliye tayari kuinyonga sheria na utu ili kutimiza malengo yake.
Mbinu alizitumia pamoja na kugoma kutoa msamaha zilikuwa tofauti na zile za maridhiano zilizotumiwa na aliyekuwa mumewe Nelson Mandela, ambaye alilenga Taifa moja tulivu, la kidemokrasia, lenye umoja na mshikamano bila kujali rangi.
Ndiyo maana haikuwa ajabu siku moja Winnie alipokaririwa akimshutumu Mandela kwa kuwasaliti weusi.
Wakati Nelson Mandela aliyerudi uraiani baada ya miaka 27 jela akitafuta maridhiano na kusameheana bila kujali namna yeye na ndugu zake weusi walivyotendwa, Winnie alitaka waliohusika na ubaguzi vitendo vya ubaguzi wa rangi waadhibiwe vikali.
“Kilichonikatili sana ninachojua ni kuchukia tu,” aliwahi kukaririwa katika mahojiano ya televisheni akisema.
Simulizi za Madikizela-Mandela ziliiteka dunia kiasi kwamba amesimuliwa katika vitabu na filamu za Hollywood, ikiwamo iliyochezwa na mshindi wa Tuzo ya Oscar, Jennifer Hudson.
Lakini pia utata wake ulisaidia kuua ndoa yake na kuharibu heshima aliyokuwa amejijengea kwa Waafrika Kusini wengi, ijapokuwa alibakia kuungwa mkono na Wazalendo weusi wenye misimamo mikali hadi mwishoni mwa uhai wake.
Baadhi walimshutumu Mandela, ambaye baada ya kutengana na mkewe huyo wa pili na kufunga ndoa na Grace Machela, Mke wa Rais wa zamani wa Msumbiji, Marehemu Samora Michale Machela kwa kuweza kuwasamehe Wazungu wakatili na wauaji akishindwa kufanya hivyo kwa mkewe huyo.
Katika miaka ya mwisho mwisho, Madikizela-Mandela, ambaye alifariki dunia Jumatatu wiki hii akiwa na umri wa miaka 81 mara kwa mara alikabiliana na mamlaka, kitu kilichozidisha kudidimiza sifa yake kama mpiganaji wa utawala wa Wazungu wachache ambao uliongoza uchumi wenye nguvu zaidi barani Afrika kuanzia mwaka 1948 hadi 1994.
Wakati mumewe akiwa jela kwa miaka 27, Madikizela-Mandela aliendesha kampeni bila kuchoka kuachiwa kwake na haki za weusi waliougulia kwa miaka mingi ya jela, vizuizini uhamishoni na kukamatwa na mamlaka za weupe.
Alibakia imara na asiyesalimu amri, akiibuka mshindi wakati alipotembea mkono kwa mkono na Mandela kutoka Jela la Victor Verster huko Capetown Feb. 11, 1990.
Kwa mume na mke, ulikuwa wakati wa furaha na kuvalishwa taji la mfalme na malkia tayari kuliongoza Taifa, kipindi kilichosababisha miaka minne baadaye kumalizika kwa karne kadhaa za utawala wa Wazungu wachache wakati Mandela alipokuwa Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini.
Lakini kwa Madikizela-Mandela, kumalizika kwa utawala wa kibaguzi, ukawa mwanzo wa mlolongo wa kesi za kisheria na matatizo ya kisiasa yakiambatana na hadithi za maisha yake ya matanuzi, kukosa uaminifu katika ndoa iliyo.
Na kuthibitisha kwa mara nyingine baada ya zama zile za utawala wa kibaguzi, katika Afrika Kusini mpya pia, kwanini jina lake la kwanza la utotoni Nomzamo lilivyomaanisha; Yule ambaye lazima akabiliwe na kesi/mitihani ya maisha.
Nomzamo Winifred Zanyiwe Madikizela alizaliwa katika familia yenye hali nzuri ya Kabila la Pondo lizungumzalo Xhosa huko Transkei.
Tarehe yake ya kuzaliwa Septemba 26, 1936, kwa mujibu wa Nelson Mandela Foundation na vyanzo vingine vingi ijapokuwa maelezo ya awali yaliutaja mwaka wa kuzaliwa kuwa 1934.
Baba yake, Columbus, alikuwa Ofisa Mwandamizi wa ile ijulikanayo nchi ya Transkei, kwa mujibu historia ya Afrika Kusini iliyopo Mtandaoni, huku nyaraka zisizo rasmi zikimtaja kuwa mtoto wa nne kati ya watoto wanane.
Maelezo mengine yanataja kuwa familia yake ilikuwa kubwa. Mama yake, Gertrude, alikuwa mwalimu ambaye alifariki dunia wakati Winnie akiwa na umri wa miaka minane.
Akiwa mtoto atembeaye pekupeku, alifuga mifugo ya familia na kujifunza kutumia vyema kile kidogo apatacho kulinganisha na mtindo wake wa baadaye wa maisha wa matanuzi.
Alihudhuria katika Shule ya Misheni ya Methodist na kisha Shule ya Ustawi wa Jamii Hofmeyr mjini Johannesburg, ambako alijenga urafiki na Adelaide Tsukudu, aliyekuja kuwa Mke wa Oliver Tambo, mshirika wa sheria wa Mandela, ambaye alienda kukiongoza chama cha African National Congress (ANC) akiwa uhamishoni.
Alipiga chini udhamini wa kwenda kusoma nchini Marekani, akichagua kubaki Afrika Kusini kama mfanyakazi wa kwanza wa Ustawi wa Jamii Mweusi katika Hospitali ya Baragwanath katika kitongoji cha Soweto.
Siku moja mwaka 1957, wakati Winnie akisubiri basi kituoni, Nelson Mandela akiendesha gari alipita hapo na kumwona. “Nilishtushwa na uzuri wake,” Mandela aliandika katika kitabu cha historia yake, “Long Walk to Freedom.”
Wiki kadhaa baadaye, anakumbuka, “Nilikuwa ofisini nilishtushwa tena wakati nilipomwona Oliver akiwa na msichana huyu kijana.”
Mandela, aliyekuwa akielekea umri wa miaka 40 na akiwa baba wa watoto watatu, akatangaza wakati wa miadi yao ya kwanza kuwa angemuoa.
Haikuchukua muda akatengana na mkewe wa kwanza, Evelyn Ntoko Mase, ambaye alikuwa muuguzi akaoana na Madikizela-Mandela Juni 14, 1958.
Madikizela-Mandela aliibuka zaidi mwaka 1964 wakati mumewe alipofungwa kifungo cha maisha jela kwa mashtaka ya uhaini.
Akapigwa rasmi marufuku chini ya sheria kali, katili na ya kibaguzi, ambayo inalenga kumfanya kana kwamba si mtu aliyepo, asiyeweza kufanya kazi, kuchangamana na jamii, kutembea hapa na pale au kunukuliwa katika vyombo vya habari vya Afrika Kusini, licha ya kwamba alikuwa akilea mabinti wao wawili, Zenani na Zindziswa.
Katika operesheni ya utawala wa makaburu wa Wazungu wachache Mei 1969, miaka mitano baada ya mumewe kufungwa jela, alikamatwa na kushikiliwa kwa miezi 17, miezi 13 katika kizuizi cha upweke. Akiwa humo alipigwa na kuteswa.
Kwa uzoefu huu wa mateso aliopitia, aliandika, ndio uliochangia kumbadili kwa kumjengea moyo wa kijasiri, usio na woga na kishari pamoja na kuwachukia sana wabaguzi na vibaraka wao.
Baada ya uasi wa weusi katika Kitongoji cha Mji wa Johannesburg cha Soweto kilichotengwa kwa ajili ya Wazalendo weusi mwaka 1976, Madikizela-Mandela kwa mara nyingine alifungwa bila kufikishwa mahakamani kwa miezi mitano.
Kisha akapigwa marufuku katika maeneo hayo na kutakiwa kuishia na kutotoka katika mji uliotawaliwa na wahafidhina wa Kizungu wa Brandfort, katika Jimbo la Orange Free.
“Mimi ni alama hai ya kinachotokea nchini,” aliandika katika kitabu cha kumbukumbu yake cha “Part of My Soul Went With Him,” ambacho kilichapwa mwaka 1984 na kuchapishwa kote duniani.
“Mimi ni alama hai ya hofu aliyonayo Mzungu. Kamwe sikubaini namna hofu hii ilivyoota mizizi hadi nilipokuja kuishi Brandfort.”
Kinyume na malengo ya mamlaka, makazi yake yakageuka mahali pa hija kwa Wanadiplomasia, Wazungu walioingiwa na huruma dhidi ya ukandamizaji weusi pamoja na wanahabari wa kigeni waliomtafuta kwa mahojiano.
Madikizela-Mandela alichangamsha mazungumzo na dunia ya nje na alikiuka vikwazo vingi alivyowekewa, akitumia simu za Wazungu pekee mitaani na kupuuza sheria zinazozuia weusi kuingia maduka ya weupe. Siku moja alipoingia katika duka la vileo na kuagiza Champagne, ujasili wake huo, uliwaacha weupe kinywa wazi.
Lakini pia kutengwa kwa Madikizela-Mandela na watu wake, kitu ambacho kilikuwa sehemu ya maisha ya kawaida nchini Afrika Kusini kulileta athari kubwa kwake na alianza kulewa sana pombe.
Wakati wa kizuizi chake hicho, nchi ilianza kubadilika hasa miongoni mwa kada la vijana. Kuanzia mwishoni mwa mwaka 1984, waandamanaji vijana waliishinikiza mamlaka kwa ujasiloi zaidi, ambao haukuwahi kuonekana.
Maandamano, machafuko na migomo ilienea na kusababisha watawala wa Kizungu kukiri kile walichosema kuwa ‘’hali ya Kimapinduzi’ na wakatangaza hali ya hatari.
Wakati Madikizela-Mandela aliporudi nyumbani kwake Soweto mwaka 1985, akivunja sheria inayomzuia kufika eneo hilo, alikuwa ni zaidi ya mwanaharakati mshari, aliyedhamiria kuchukua uongozi wa kile kilichokuwa awamu mpya harakati za kimaamuzi na ghasia zaidi.
Kama alivyoiona, jukumu lake liliimarishwa na kukomazwa na makabiliano yake ya mara kwa mara na mamlaka.
“Pamoja, kwa mshikamano na maboksi yetu ya vibiriti na mikufu yetu, tutaikomboa nchi hii,” aliuambia mkutano wa hadhara Aprili 1986.
Alitumia neno ‘mikufu’ fumbo lililomaanisha aina ya uuaji wa kutumia taili lililochovywa kwenye gesi kisha kuliingiza katika shingo za wasaliti, mbinu, ambayo ilileta mshituko mkubwa kwa kizazi kikongwe cha wanaharakati wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Lakini aliendelea kushikamana na kuwaongoza vijana wenye misimamo mikali mjini humo ambao walihakikisha kufanikiwa kwa dhamira yao bila kujali ukatili wa mbinu zao hizo.
Mwishoni mwa miaka 1980, Madikizela-Mandela aliruhusu makazi yake ya Soweto kutumiwa na kile kilichojulikana kama Mandela United Football Club, genge la kikatili lililodaiwa kuwa walinzi wake. Ni genge lililoisumbua mno Soweto na kukaribisha hofu na mauaji.
Mwaka 1991 alitiwa hatiani kwa kuamuru kutekwa kwa vijana wanne wa Soweto 1988.
Mwili wa mmoja wao 14, aliyeitwa James Moeketsi Seipei maarufu kama Stompie, neno lililotokana na umbo lake fupi, ulikutwa ukiwa umekatwa koo.
Inasemekana aliuawa na kuteswa kwa kile kilichoelezwa kuwa aliwasaliti wazalendo weusi kwa kupenyeza siri zao kwa polisi wa makaburu.
Mlinzi Mkuu wa Madikizela-Mandela alitiwa hatiani kwa mauaji hayo na Winnie akapewa adhabu ya kifungo cha miaka sita jela kwa utekaji nyara, lakini Mahakama ya Juu ya Rufaa ya Afrika Kusini ilipunguza adhabu hiyo kuwa faini na kifungo cha nje cha mwaka mmoja.
Katika kipindi hicho kilichoanza kuathiri umaarufu wake, The United Democratic Front, kundi mwavuli lililoleta pamoja vuguvugu za kupambana na ubaguzi wa rangi na ambalo lilihusishwa na ANC, lilimtimua.
Aprili 1992, Mandela, kupitia mazungumzo yake ya kufikia makubaliano na Rais wa mwisho wa Afrika Kusini ya kibaguzi, . W. de Klerk of South Africa, alieleza nia yake ya kutengana na mkewe kwa kile kilichoelezwa kutembea na mwanasheria mmoja kijana.
Winnie mwenyewe alipuuza dhana kwamba alitaka kujulikana kama ‘Mke wa Rais’. ‘Mimi si aina ya mtu wa kubeba maua mazuri na manukato kwa kila mtu,” alisema.
Miaka miwili baadaye, Mandela alichaguliwa kuwa Rais na alimpatia Winnie kazi ya Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni, Sayansi na Teknolojia.
Lakini baada ya tuhuma za kutumia ushawishi wake vibaya, kupokea rushwa na kutumia vibaya fedha za Serikali, ikiwamo kusafiri kwenda Ghana bila ruhusu, aling’olewa ofisini.
Mwaka 1996, Mandela alihitimisha ndoa yao ya miaka 38, akitoa ushahidi mahakamani namna mkewe alivyokuwa akimsaliti.
Mwaka uliofuata, mbele ya Askofu Desmond M. Tutu katika Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Afrika Kusini Madikizela-Mandela aliomba radhi kwa matukio ya mwishoni mwa miaka ya 1980. “Vitu vilienda mrama,” alisema na kuongeza, “Kwa hilo ninasikitika na kuomba radhi.”
Lakini bado utata uliendelea kumfuata. Mwaka 2003 alitiwa hatiani kwa kutumia nafasi yake ya Urais wa Wanawake wa ANC kujipatia mikopo isiyo halali; alipewa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela. Lakini kifungo chake kilisimamishwa kwa rufaa, baada ya Jaji kuona kuwa hakunufaika binafsi kwa miamala ya fedha.
Hadi mwisho Madikizela-Mandela alibakia mwanasiasa aliyeigawa jamii, akipendwa na wafuasi wake, waliokuwa tayari kumtetea wakijikita na mchango wake mkubwa kuhitimisha utawala wa kibaguzi, lakini pia akizungumzwa vibaya na wakosoaji ambao walimuona kuwa mchafu.
Wachache hata hivyo waliweza kupuuza matukio mengi yenye utata ambayo hayakupatiwa jawabu.
Kwamba Mke huyo wa Pili wa Mandela anajulikana zaidi kama Mwanaharakati, Mwanamapinduzi na shujaa, haijalishi mambo machafu aliyohusika nayo.
Viongozi mbalimbali duniani, AU, UN waomboleza
Viongozi mbalimbali duniani wameendelea kutoa salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha Winnie Madikizela-Mandela.
Mandele alifariki katika Hospitali ya Netcare Milpark baada ya kuugua kwa muda mrefu, akilazwa hospitali mara kwa mara tangu kuanza kwa mwaka huu kwamba alifariki akiwa amezungukwa na familia yake.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC), Winnie alilazwa hospitali mwishoni mwa wiki iliyopita akilalamika mafua baada ya kuhudhuria ibada ya Ijumaa Kuu. Alitibiwa kisukari na kufanyiwa operesheni kubwa wakati afya yake ikizorota kipindi cha miaka kadhaa.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema amesikitishwa na kifo cha Winnie na amemuelezea kama mwanamke shupavu na imara katika harakati za ukombozi wa Afrika Kusini.
Akizungumza baada ya kuizuru nyumba ya Winnie mjini Soweto, Ramaphosa amesema mwanamama huyo ameacha urithi mkubwa na aliyagusa maisha ya mamilioni ya Waafrika Kusini katika kipindi cha giza cha utawala wa kibaguzi wakati chama cha ANC kilipopigwa marufuku.
”Aliendelea kuonyesha ujasiri dhidi ya mifumo yote ya kutisha. Ni mtu ambaye amepitia mateso na misukosuko mingi na kifo chake ni pigo kubwa. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha Waafrika Kusini wengi wa rangi na itikadi tofauti za kisiasa,” alisema Ramaphosa.
Ameongeza kusema kuwa Winnie ni shujaa wa haki na usawa na sauti kwa wasio na sauti.
Ramaphosa amesema ibada rasmi ya kumbukumbu itafanyika Aprili 11 na mazishi ya kitaifa yatafanyika Aprili 14.
Tangu kifo hicho kilipotokea, umati wa watu umekusanyika nje ya makazi ya Winnie wakiimba na kucheza nyimbo za kuomboleza.
Askofu Mkuu Mstaafu wa Afrika Kusini Desmond Tutu, amesema Winnie ni jasiri katika historia ya vizazi vya wanaharakati ambaye alikataa kuwasujudia waliomfunga mumewe.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat amesema umoja huo unaungana na Bara lote la Afrika kuomboleza kifo cha Winnie ambaye siku zote atakumbukwa kama mwanaharakati asiye na woga na aliyejitoa maisha yake kwa ajili ya kupigania Uhuru wa Afrika Kusini na wanawake wote kwa ujumla.
Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea kusikitishwa na kifo hicho akisema kuwa mama huyo alikuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Guterres amesema Winnie alizungumza bila kuwa na hofu katika kutetea haki sawa.
Kwa upande wake, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari amesema Winnie atabakia kuwa tunu si tu ya mwanamke wa Kiafrika, bali Waafrika wote kwa ujumla.
Naye kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, amesema Winnie aliongoza mapambano dhidi ya utawala wa kikatili wa ubaguzi wa rangi na aliwahamasisha wanawake ulimwenguni kote kuingia katika maeneo ya mapambano kudai haki na Uhuru.
Watu mashuhuri waliotoa salamu za pole ni pamoja na Mwanaharakati wa Haki za Kiraia, Jesse Jackson, mwigizaji maarufu Idris Elba na Mwanamitindo wa Kimataifa, Naomi Campbell.