GENEVA, USWISI
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa zaidi ya maambukizi 106,000 yameripotiwa kwa siku moja juzi, hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi kwa siku tangu mripuko wa virusi vya corona katika mji wa Wuhan huko China mwezi Desemba.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alismajana kuwa ana wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali katika mataifa masikini duniani.
Idadi hiyo mpya ambayo ni kubwa kuwahi kurekodiwa inatajwa kuwa inatokana na nchi nyingi kuboresha na kuongeza huduma za upimaji wa maambukizi ya virusi hivyo vya corona.
“Bado tuna safari ndefu katika kupambna na maambukizi ya gonjwa hili. Tunafuatilia wka karibu kuhusu ongezeko la maambukizi hasa katika nchi za uchumi wa kati na zile masikini zenye uchumi wa chini,” alisema Tedros.
Zaidi ya watu milioni 4.9 ameripotiwa kuambukizwa virusi vya corona tangu ulipoibuka nchini China Desemba 2019, kwa mujibu wa takwimu zilizorekodiwa na shirika la habari la AFP.
Hadi sasa, tayari watu 325,000 wameripotiwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kunulikiw ana AFO.
Jumanne wiki hii WHO ilitangaza kuruhusu kufanyiwa uchunguikuhusu naman ilivyoshughuliki janga hilo baada ya tuhuma kutoka kwaRais wa Marekani, Donald Trump ambaye alidai kuwa shirikahilo halikutenda ipasavyo na lilitumika kisiasa kwa manufaa ya China.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Trump kuiandikia barua WHO akisema shirika hilo halikuchukua hatua stahiki na kwamba iwapo halitakubali kuchunguzwa ndani ya siku 30 zijazo Marekani itaondoa ufadhili wake na kuangalia uwezekano wa kujivua uanachama wa shirika hilo.
Marekani ndiyo mchangiaji mkubwa wa bajeti ya WHO na tayari ilishatangaza kusitisha uchangiaji wake kwa muda.
Hata hivyo, katika rekodi Bara la Ulaya linaonekana kuwa limevuka kilele cha maambukizi huku idadi ya visa vipya na vifo ikionekana kushuka kila siku jambo linalotoa nafasi kwa baadhi ya nchi kulegeza vikwazo vyake.
Urusi Jumatano ilirekodi kiasi kidogo zaidi cha maambukizi tangu Mei Mosi huku wagonjwa wengi wakiruhusiwa kutoka hospitali na kurudi nyumbani. Kulingana na maofisa nchini Urusi, hii inaonyesha kwamba maambukizi hayaongezeki tena kwa sasa.
Nchini Italia viwanja vya ndege vimeruhusiwa kufunguliwa tena kuanzia Juni 3 ambapo ndege za kimataifa pia zitaingia nchini humo.
Huko Amerika ya Kusini nako, hali imezidi kuwa mbaya zaidi nchini Brazil na taifa hilo huenda likawa la pili duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi.
Nchi hiyo ilitoa mwongozo kwa raia wake kutumia dawa ya kutibu malaria Hydroxychloroquin katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.
“Daktari ndiye anayeamua kumpa mgonjwa dawa hiyo, na mgonjwa ana haki ya kuikubali au kuikataa. Tunawafahamisha kabisa kuhusiana na athari zake,” alisema ofisa katika Wizara ya Afya Brazil, Mayra Pinheiro.
Barani Asia nako maambukizi nchini Japan yanapungua na nchi hiyo italegeza baadhi ya vikwazo katika miji ya Osaka, Kyoto na Hyogo Alhamis.
Thailand ilisema inatarajia chanjo ya virusi vya corona iwe tayari mwakani, baada ya majaribio yaliyofanyiwa panya kuonyesha matumaini.
Barani Afrika, Wizara ya Afya Afrika Kusini imeripoti kifo chake cha kwanza kinachohusiana na corona kwa mtoto mchanga wakati ambapo idadi ya vifo nchini humo imefikia watu 339.
Huku idadi ya maambukizi na wanaofariki ikiongezeka kote duniani kila uchao, serikali zinataraji kwamba chanjo itapatikana hivi karibuniili ziweze kuzinusuru chumi ambazo zimeathirika vibaya.
Ila kulikuwa na habari ya kutia moyo Jumatano, kwani tafiti zilizofanyiwa tumbili zilionyesha kwamba binadamu wanaweza kupata kinga dhidi ya virusi vya corona.