WASHINGTON, MarekaniÂ
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limefurahishwa na matokeo ya awali ya najaribio ya dawa ya kutibu corona Uingereza yanayoonesha dawa ya dexamethasone, inaweza kuokoa maisha ya watu walio mahututi wanaougua ugonjwa wa Covid-19.
Kwa wagonjwa wanaotumia mashine za kupumua, dawa hiyo ilionesha kupunguza idadi ya vifo kwa theluthi moja na kwa wagonjwa wanaohitaji hewa ya oksijeni, idadi ya vifo ilipungua kwa humsini au moja ya tano kulingana na matokeo ya awali yaliyotolewa na shirika hili.
Hata hivyo, faida ama uzuri wa dawa hiyo kulijitokeza kwa wagonjwa wanaoumwa sana kwa sababu ya virusi vya corona wala sio kwa wenye athari za wastani za ugonjwa huo.
“Hii ndio dawa ya kwanza kupunguza idadi ya vifo kwa wagonjwa wa virusi vya corona wanaohitaji oksijeni au walio kwenye mashine za kupumua,” alisema Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus.
“Hii ni habari njema na ninapongeza serikali ya Uingereza, Chuo Kikuu cha Oxford, na hospitali nyingi na wagonjwa Uingereza ambao wamechangia utafiti huu wa kisayansi ambao ni mwokozi wa maisha.”
Dexamethasone ni dawa ambayo imekuwa ikitumiwa tangu mwaka 1960 kupunguza uvimbe katika hali tofauti kama vile ugonjwa wa saratani, yabisi kavu na kadhalika.
Watafiti walishirikishana maoni yao ya awali kuhusu matokeo ya majaribio ya dawa hiyo na WHO, huku wakitarajia utafiti wa kina wa data siku za hivi karibuni.
Dawa ya bei rahisi inayopatikana kwa urahisi Dexamethasone, inaweza kusaidia maisha ya wagonjwa wa virusi vya corona waliopo katika hali mahututi.
Wataalamu wa Uingereza wanasema tiba hiyo yenye steroid ni hatua kubwa iliopigwa kukabiliana na virusi hivyo hatari.
Dawa hiyo, ni miongoni mwa majaribio ya tiba ya corona duniani kuona iwapo inaweza kusaidia kutibu corona.
Watafiti wanakadiria, iwapo dawa hiyo ingekuwepo nchini Uingereza kuanzia mwanzo wa mlipuko wa corona , hadi maisha ya watu 5,000 yangeokolewa.
Kwa sababu ni ya bei rahisi inaweza kuyasaidia pakubwa mataifa masikini yanayotatizika katika kukabliana na ugonjwa wa Covid-19.
Inaokoa maisha
Kati ya wale waliolazwa hospitalini , wengi wao hupata nafuu , lakini wengine wangehitaji oksijeni ama mashine za kuwasaidia kupumua .
Hawa ni wagonjwa ambao wapo katika hali mahututi na wanasaidiwa na dexamethasone.
Katika majaribio hayo yalioongozwa na Chuo Kikuu cha Oxford , takriban wagonjwa 2,000 wa hospitali walipatiwa dexamethasone na walililangishwa na wengine 4,000 ambao hawakupatiwa tiba hiyo.
Kwa wagonjwa waliokuwa katika mashine za kuwasaidia kupumua ilipunguza hatari ya kufariki kutoka asilimia 40 hadi 28 . Kwa wagonja waliohitaji oksijeni ilipunguza hatari ya kifo kutoka asilimia 25 hadi 20.
Mchunguzi Mkuu, Profesa Peter Horby alisema: Hii ndio dawa pekee kufikia sasa ambayo imeonesha kupunguza hatari ya kifo na inapunguza kwa kiwango kikuu., ”ni mafanilkio makubwa”.
Profesa landray alisema Hospitali zinapaswa kuitumia bila kuchelewa lakini watu hawafai kuinunua ili kupeleka nyumbani.