LONDON, ENGLAND
KLABU ya West Ham imepanga kumtoza faini ya pauni 200,000 (sawa na Sh milioni 594 za Kitanzania) mshambuliaji wake, Marko Arnautovic, kwa kosa la kuonyesha utovu wa nidhamu.
Kutokana na sababu hiyo inayodaiwa ni kushinikiza uhamisho wake nchini China, nyota huyo aliondolewa katika kikosi kilichocheza dhidi ya Bournemouth.
Arnautovic amesisitiza anataka kuondoka mwezi huu baada ya kujitokeza klabu ya Shanghai SIPG inayocheza Ligi Kuu ya China, lakini West Ham imegoma kumuuza nyota huyo hadi watakapopata mbadala wake.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Stars, uamuzi huo umeonekana kumwathiri mshambuliaji huyo baada ya Shanghai SIPG kuwa tayari kuweka mezani dau nono.
Kutokana na sababu hizo Kocha wa West Ham, Manuel Pellegrini, alimwondoa nyota huyo katika kikosi chake kilichopangwa kucheza jana dhidi ya Bournemouth.
West Ham inadaiwa kuhitaji pauni milioni 45 baada ya kukataa ofa ya pauni milioni 35 kutoka Shanghai SIPG.
Pellegrini alisisitiza kuwa: “Arnautovic, alifanya mazoezi wiki nzima bila tatizo lolote lakini ghafla alitoweka klabuni.”
Kutokana na kitendo hicho, Arnautovic aliwaomba radhi wachezaji wenzake lakini hakuficha hisia zake kwamba anataka kuondoka jambo ambalo kocha wa timu hiyo alitaka klabu hiyo kutafuta mwarobaini wa tatizo hilo haraka.
Akizungumzia sakata la mchezaji huyo, Pellegrini alidai: “Marko ni mmoja kati ya wachezaji muhimu lakini vijana wangu wanafahamu kuwa kuna kitu kitatokea.”