MWANDISHI WETU
WENYEVITI wa Mashina wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuhakikisha wanapanga ulinzi unaofaa katika maeneo yao ili kukomesha wizi wa televisheni aina ya flat screen uliokithiri Kivule wilayani Ilala na wasipofanya hivyo watashtakiwa kwenye chama.
Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kerezange, Ismail Ibrahimu katika kikao kati ya viongozi na wananchi.
Kikao hicho kimefanyika baada ya wananchi katika maeneo hayo kulalamikia vitendo vya wizi wa televisheni unaonyika kwa kukata madirisha kukithiri katika maeneo yao.
Akitoa muongozo baada ya wananchi kushindwa kufikia uamuzi wa utaratibu gani watatumia kukabiliana na wimbi hilo la wizi, alisema kila Mwenyekiti wa Shina akae na watu wake kupanga utaratibu unaofaa kwa ajili ya ulinzi.
“Mkakae na wakazi wenu mpange namna ya Ulinzi unaofaa, mtakayokubaliana tuleteeni utakuwa utaratibu tutakaousimamia.
“Wenyeviti wa mashina wanatoka CCM, kwa mujibu wa taratibu za chama wenyeviti wa mashina watakiwa kutimiza wajibu wao katika suala zima la ulinzi.
“Wasipotekeleza tutashtakiana kwenye chama kwa sababu mtakuwa mmeyatelekeza majukumu yenu, fanyeni katika ngazi ya mashina,”alisema Mwenyekiti Ismail.