NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuonya Msanii wa Filamu nchini, Wema Sepetu na kumtahadharisha kwamba akirudia kuvunja masharti mahakama haitasita kumfutia dhamana.
Uamuzi wa mahakama hiyo ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde ambapo Wema alifika mahakamani hapo akitokea gerezani kwa ajili ya kusikiliza endapo atafutiwa dhamana ama la.
Wema alikuwa gerezani Segerea tangu Juni 17 mwaka huu mahakama hiyo ilipoamuru akisubiri uamuzi wa jana ambao ulikubali mshtakiwa huyo kuendelea kuwa nje kwa dhamana.
Akisoma uamuzi Hakimu Kasonde alisema Juni 17 mwaka huu mshtakiwa alifikishwa mahakamani akiwa chini ya ulinzi ili ajieleze kwanini dhamana yake isifutwe.
“Wakili Albert Msando aliwasilisha hati ya kiapo kuelezea sababu ya mshtakiwa kutofika mahakamani Juni 11 mwaka huu.
“Baada ya kufikiria kwa kina sababu zilizotolewa katika hati ya kiapo na maelezo ya mshtakiwa inaonekana ni kweli mshtakiwa alivunja masharti ya dhamana yake.
“Sababu kubwa walisema ni kuugua ghafla, Kiubinadamu hali hiyo inaweza kutokea, swali kwanini kama alikuwa eneo la mahakama hakufanya mawasiliano.
“Mahakama inakuonya kuhakikisha pale ambapo haupo mahakamani ijulishe kupitia wadhamini wako na si vinginevyo, wakili hachukui majukumu ya wadhamini, kila mmoja anawajibika kivyake,”alisema.
Alisema mahakama inatoa onyo kwa washtakiwa, ikitokea akarudia alichofanya haitasita kumfutia dhamana. Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Julai 4 mwaka huu.