23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI WA JK AELEZA MACHUNGU YA KULALA SELO

Na ELIZABETH HOMBO -DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika serikali ya awamu ya nne, Lawrence Masha, amesimulia alivyopitia machungu ya kulala selo wakati akiwa Chadema.

Alisema  kukaa eneo hilo ni zaidi ya kuonana na mtu kama Osama Bin Laden.

Masha   alirejea CCM hivi karibuni akitokea Chadema, alipohamia kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Alisema  akiwa upinzani alikamatwa mara kadhaa na polisi na kulala katika Kituo cha Polisi Oysterbay Kinondoni, baadaye kupelekwa Segerea na mara ya mwisho alishikwa akiwa mjini Mpanda na kulala ndani.

Masha alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA   nyumbani kwake Mikocheni   Dar es Salaam juzi.

Alipotakiwa kueleza uzoefu wake wa kukamatwa na polisi akiwa upinzani alisema : “Nilikiona cha mtema kuni, ni zaidi ya kuonana na Osama Bin Laden.

“Niliwekwa ndani pale Oysterbay polisi na kama Mwigulu (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,   Nchemba) ananisikiliza pabadilishwe ,hapafai pale, nimekaa pale for one night (usiku mmoja) lakini nilikipata.

“Nikakimbizwa kesho yake kwenda Kisutu nikanyimwa dhamana, nikalala Segerea, kimsingi ninachotaka kusema haya mambo yanatokea katika mapambano yoyote na yamenipata.

“Mpanda nilikuwa nina kesi nikawa naenda kila mwezi namshukuru Mungu kuwa nilishinda kesi zote.

“Mwisho wa siku kila mtu anajua ukiongea na kukitaka chakula cha mwenzako utashughuliwa hivyo ulitambue hilo, mimi si nilishughulikiwa!” alisema Masha.

Agosti 25, 2015 Masha alipandishwa kizimbani akikabiliwa na shtaka la kutumia lugha ya matusi kwa maofisa wa   polisi.

Alidaiwa Agosti 24,2015  katika Kituo cha Polisi cha Osterbay alitoa lugha ya matusi kwa maofisa wa jeshi la polisi.

AZUNGUMZIA MAISHA YAKE YA SIASA

Pamoja na mambo mengine, Masha aliyepata kuwa Mbunge wa Nyamagana mkoani Mwanza,  alisema amekulia katika familia ya siasa na kitu ambacho amefundishwa ni kuipenda nchi yake.

“Nimefundishwa kufanya kile ambacho naona ni sahihi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yangu, leo hii tunavyoongea sioni sababu ya kujiunga na chama chochote cha upinzani,”alisema.

Alisema hana sababu ya kukihama tena chama hicho tawala kwa sababu Rais Magufuli anafanya kazi ambayo wananchi wamekuwa wakiomba ifanyike kwa muda mrefu.

“Sisi wengine katika shughuli tunazozifanya hatufanyi kwa ajili ya kutafuta kitu au tunataka kitu, tunafanya kwa ajili ya maendeleo ya watoto wetu na watanzania.

“Imani yangu ni kwamba Rais Magufuli ana nia njema na nchi na kazi anafanya, suala la kuniuliza sijui baada ya miaka 50 nitafanya nini nafikiri ‘is not a fair question’.

“Lakini kama nilivyoeleza siku ile nilivyokubaliwa ndani ya chama changu cha zamani mimi hapa nitakuwa mwaminifu kwa CCM na nitakuwa mwaminifu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”alisema.

Alipoulizwa kuwa miezi michache akiwa Chadema alipata kuzungumza na vyombo vya habari akisema nchi inaendeshwa kwa kutofuata sheria na kwamba je amebadilisha kauli yake?

Alisema:”Sikumaanisha hivyo bali nilisema pamoja na nia njema sheria ifuatwe.

“Pamoja na nia njema uliyonayo unaweza kuruka kabla hujatakiwa kufika pale unapotakiwa kwenda.

“Kikubwa ambacho kinatakiwa kufanyika ni kwamba kwanza washauri wake wa karibu na yeye mwenyewe atambue kwamba tunayo katiba tunazo sheria za nchi hii na zinatakiwa kufuatwa.

“Ukizifuata inasaidia kwa sababu kesho na keshokutwa hakuna mtu ambaye anaweza kuuliza kwa nini hili lilifanyika.

“Nilipojiunga na CCM, hata juzi hapa nilisema katika maongezi mbalimbali tofauti, Magufuli si malaika ni binadamu lakini ana nia njema na nchi.

“Kukosea au kupoteza step kidogo wakati mwingine siyo kosa lake yeye ana watu ambao wanatakiwa kumshauri aweze kufika pale alipo na kule anapotaka kwenda.

“Kikubwa tunachotakiwa kuangalia ni dhamira ya mtu ni kipi anachotaka kukifanya kwa ajili ya watu wake, na wataalamu wamsaidie kuhakikisha kwamba tunafuata process ambazo zinatakiwa kufuatwa.”

ATOA MAMBO MATATU KWA WASHAURI WA RAIS

Alipoulizwa endapo wataalamu wa Rais wanamshauri vizuri, alisema tatizo ambalo analiona hivi sasa, anajua nafasi ya rais ni kubwa sana na anaamini kwamba kuna watu wengi wanamwogopa.

“Na kwa bahati nzuri au mbaya rais amekuwa serikalini hivyo anajua ujinga ambao unafanyika serikalini na mimi nimekaa serikalini nafahamu vizuri.

“Hivyo anatakiwa kuwa na watu ambao kwanza wanamheshimu, pili ni wawe wataalamu kweli, tatu wawe wanamweleza ukweli. Hicho ndicho kinachotakiwa,”alisema.

 

ASEMA ATAENDELEA KUMHESHIMU LOWASSA

Masha ambaye alijiunga na Chadema akimfuata  Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye jina lake lilikatwa katika kura za maoni za kugombea urais ndani ya CCM, alisema ingawa  amekihama Chadema lakini ataendelea kumheshimu Mbunge huyo wa zamani wa Monduli.

Alisema katika uamuzi huo wa kurudi CCM, hakumshirikisha Lowassa na   bado hajawasiliana naye.

“Sikumweleza na sikumuaga, nilisema nitaendelea kumheshimu kama mzee wangu na atakayesema simheshimu mzee Lowassa atakuwa ni mwehu.

“Ni baba yangu sijamuaga na sijaonge naye hadi leo hii, lakini kila mtu ana akili yake kwamba kinachofanyika hivi sasa CCM ni sawa lakini kinachofanyika Chadema  sawa.

“Lakini atabaki kuwa baba yangu nitaendelea kumheshimu,”alisema Masha.

 

AMZUNGUMZIA LISSU

Masha pia amesema si fedheha kwa Serikali kuomba msaada wa uchunguzi kutoka nje   kuchunguza tukio la kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Kauli hiyo ya Masha   inapingana na   ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

Nchemba    alipata kueleza kuwa kuomba msaada wa uchunguzi nje ya nchi litakuwa jambo la mwisho.

“Tusingependa kuitangazia dunia kuwa jukumu la kulinda raia wetu limetushinda, hili litakuwa jambo la mwisho na lazima damu inayomwagika adhabu yake iwe kubwa zaidi,” alisema Mwigulu wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari miezi miwili iliyopita.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili (TLS) anauguza majeraha katika Hospitali ya Nairobi,  Kenya, kwa takribani miezi mitatu baada ya kupigwa risasi lakini hadi sasa vyombo vya dola vimeshindwa kuwabaini waliotenda tendo hilo la kinyama.

, Masha alisema Serikali ikileta watu wa upande wa pili kuongeza nguvu labda watu wangekuwa na imani.

“Naamini jeshi letu linaweza kufanya uchunguzi lakini pia siyo fedheha kuomba msaada. Ilitokea Kenya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Robert Ouko ambaye alipotea lakini ukafanyika uchunguzi kutoka nje.

“Huwezi ukamtakia mabaya mtu aliyepata matatizo kama Lissu, ndiyo maana hata juzi Samia (Makamu wa Rais, Suluhu Hassan) alimtembelea hospitalini Nairobi.

“Tutakuwa nchi ya wanyama kama Mtanzania mwenzetu anapatwa na matatizo halafu unakosa utu wa kusema kwamba huyu nimjali, nimfuate, nimtakie mema.

“Unajua nimekaa kwenye siasa kwa muda mrefu hata kama mnashindana kwenye siasa huwezi kumfanyia mtu vile kama alivyofanyiwa Lissu.

“Tungeleta hawa watu wa upande wa pili wa kuongeza nguvu labda watu wangekuwa na imani,” alisema Masha.

Alisema si kweli kwamba ndani ya Jeshi la Polisi wote ni wabaya kama watu wengi wanavyodhani bali kuna vijana wazuri ambao wanafanya kazi kwa weledi.

“Hawa wanaosema jeshi lote la polisi ni baya huwa siwaelewi, sasa ina maana kesho au keshokutwa ukichukua nchi utaweza kubadili jeshi lote la polisi?

“Utamtoa wapi IGP kama si hawa waliopo, huwezi kuniambia ndani ya jeshi la polisi watu wote ni wabaya,” alisema Masha.

Tangu Lissu aliposhambuliwa chama chake  cha Chadema   na familia yake, wamekuwa wakiomba Serikali kuomba msaada wa uchunguzi kutoka nje ya nchi ili kuondoa utata uliopo.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, amelazwa katika Hospitali ya Nairobi akitibiwa majeraha ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7, mwaka huu nje ya nyumba yake  Area D, mjini Dodoma wakati akirejea kutoka bungeni.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

 1. Kwanza umezungumzia mateso. Pili umemzungumzia Lowassa. tatu umemzungumzia Lisu.
  Inaonekana wazi,Umeumizwa na kudharalishwa.
  Unajua wazi walio karibu na Raisi hawana vigezo na wengi wanamwogopa. Umekiri hapa anavitisho, hana uhuru. na walio karibu hawana elimu mbadala kuwa karibu naye.
  Umesema utamheshimu Lowassa. Unajua anahadhi,/.
  Ni wazi na umeungama yote yanayosemwa na wapinzani.
  Umekuwa mwoga, umeogopa mateso, unamjua ndugu magufuli hajaweka uhuru kwa kufanya kazi na watu aliowateua . Ni Amri tupu ndo maana wanamini.
  Uhuru. akubali uchunguzi toka nje. Haya yote ni mapungufu makubwa na umekuwa mwoga umeamua kutuliza moyo CCM. Huhitaji kitu. Acha uongo. Ungebaki kule kuhakikisha na kumshauri arekebishe hayo kwa ajili ya Watanzania. Unajifunga mwenyewe, Nawe pia dhaifu. Kama ulivyoyaona ya mkuu, nayaona mapungufu hayohayo kwako,
  Umesarenda. Nilikutegemea kati ya wengi. Umeliangusha Taifa na uhuru na uzalendo uliousimamia. Utapewa cheo tu. Na ni aibu kwa msomi kama wewe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles