Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi karika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama amesema Serikali peke yake haiwezi kujenga Makao Makuu ya nchi Dodoma.
Amesema inahitaji ushirikiano wa Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF).
Mhagama aliyasema hayo jana alipokuwa mgeni rasmi katika mkutano wa bodi ya TPSF ambako mengi yalizungumzwa kuhusu kuhamia Dodoma.
“Safari ya Dodoma imeiva na maandalizi yamekamilika, sisi Serikali peke yetu hatuwezi kujenga makao makuu ya nchi Dodoma, tunahitaji sekta binafsi.
“Tunakamilisha taratibu za bbunge kuipeleka sheria ya kutambua Dodoma ni Makao Makuu ya nchi ili ipitishwe.
“Itasaidia kuongoza Serikali, itaondoa migogoro na itaweka mfumo wa kuiwezesha TPSF kutengeneza mazingira bora ya Dodoma,”alisema.
Alisema sekta binafsi inatakiwa kutambua fursa zilizopo Dodoma na kama inafikiri kuna uwezekano wa kujenga viwanda haraka ifanye hivyo, Serikali iko tayari na maeneo yapo.
“Tumewaagiza Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) wasifanye urasimu wa aina yoyote.
“Atakayehitaji kiwanja kwa ajili ya kujenga hoteli apewe kiwanja ndani ya wiki moja na ajenge siyo akae nacho miaka 30 kama wanavyofanya wengine,”alisema.
Aliwaomba wawekezaji waende Dodoma kujenga shule kwa vile kutakuwa na ongezeko la watu kati ya 900,000 mpaka milioni moja hivyo shule binafsi zinahitajika kujengwa kama ilivyo Dar es Salaam.
Akizungumzia mahitaji ya Dodoma, Mkurugenzi wa CDA, Paskas Muragili alisema sekta binafsi haina budi ichangamkie fursa ya kujenga shule, soko lenye hadhi ya kubwa ya kimataifa ikizingatiwa yaliyopo ni madogo.