Na Munir Shemweta, WANMM SERENGETI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameitaka jamii ya wafugaji wilayani Serengeti mkoani Mara kuachana na utaratibu wa zamani wa ufugaji wa kuhamahama na mifugo na badala yake waendeshe ufugaji wa kisasa uliojikita kibiashara.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bisarara katika Hhalmashauri ya wilaya ya Serengeti mkoani Mara wakati wa ziara ya Mawaziri 8 wa Wizara za Kisekta kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 mwishoni mwa wiki, Ndaki alisema kwa sasa upungufu wa ardhi ya kuchungia mifugo ni mkubwa kwa kuwa idadi ya watu na mifugo kuongezeka lakini ardhi haiongezeki.
Alisema, kutokana na hali hiyo kuna haja kwa jamii ya wafugaji nchini kuanza kubadilika kwa kuacha kuendelea na utaratibu wa zamani wa kuhama na mifugo kutoka eneo moja kwenda lingine ulioonekana kuzua migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
“Katavi, Rukwa, Mbeya, Lindi mpaka Mtwara wafugaji wamejaa na malisho haayatoshi hivyo tusipofanya ufugaji wa kuvuna mifugo yetu tutaifugia wapi,” amesema Ndaki.
Kwa mujibu wa Waziri Ndaki, ni vyema kuanzia sasa wafugaji wakà angalia namna bora ya kubadilika kwa kufanya ufugaji wa kuvuna alioueleza kuwa utawezesha jamii hiyo ya wafugaji kutumia sehemu ya fedha kwa shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri 8 wa Wizara za Kisekta aliwaeleza wananchi wa kijiji cha Bisarara wilayani Serengeti mkoa wa Mara kuwa, ni vizuri maeneo ya vijiji yaliyorasimishwa kutoka hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupangiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi utakaoainisha maeneo ya kufugia na kulima ili kuepuka migogoro ya ardhi
Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema, wakazi wa vijiji vilivyobakishwa kwenye maeneo ya hifadhi ya Serengeti kuhakikisha shughuli zinazofanyika pembezoni mwa mipaka ya hifadhi kuwa za ufugaji badala ya kilimo ili kuepuka uharibu unaoweza kufanywa na wanyama.
Mbunge wa Jimbo la Serengeti Dk. Amsabi Mrimi alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuwajali wananchi wa vijiii kwa kuwapatia sehemu ya ardhi ya hifadhi na kueleza kuwa mtu anayetoa ardhi kwa wananchi anakuwa amewasaidia sana kwa kuwa ardhi ndiyo kila kitu.
Aliishauri serikali kupitia upya sheria ya kuhamisha mifugo kwenye maeneo ya vijiji vilivyopo kando ya hifadhi kwa kueleza kwamba sheria hiyo imeleta madhara makubwa kwa jamii ya wafugaji.