28 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Ndaki ataka kuainishwa mipaka ya hifadhi ya bahari kuu

Na Edward Kondela, Pwani

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amekitaka Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kuhakikisha hadi kufikia Agosti mwaka huu kinaweka alama za mipaka katika maeneo yote ya hifadhi za bahari ili kuondoa migogoro kati yao na wavuvi.

Akizungumza jana Februari 23, na wananchi katika Kata ya Jibondo iliyopo Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani, Waziri Ndaki ametaka kuwekwa kwa alama za mipaka hiyo baada ya baadhi ya wananchi kulalamikia kutozwa faini mara kwa mara kwa tuhuma za kufanya shughuli za uvuvi kwenye maeneo hayo ambayo hayaruhusiwi kisheria kwa shughuli hizo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati) akijadiliana jambo na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dk. Rashid Tamatamah wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Aidha, Waziri Ndaki akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Pauline Gekul, amewataka wavuvi kuhakikisha pindi wanapokamatwa kwa makosa mbalimbali ambayo ni kinyume na sheria ya uvuvi kuhakikisha wanapatiwa risiti inayotambulika na serikali ya kieletroniki (EFD) na kuonya watumishi wa serikali wanaopokea fedha za faini bila kutoa risiti hizo.

“Tuweke mipaka ya hifadhi ieleweke hapa ndiyo mwanzo na hapa ndiyo mwisho, hadi mwezi wa nane maeneo tengefu yawe na mipaka yake ya hifadhi ya bahari, pia tushirikishe wananchi na viongozi wao siyo kuweka tu mipaka, pia kwa mtu anayekutwa na kosa la kwenda kinyume na sheria ya uvuvi akilipa faini apewe risiti ya serikali ya kieletroniki (EFD),” amesema Ndaki

Pia, uNdaki ametaka kufanyika kwa utafiti zaidi ndani ya mwezi mmoja juu ya matumizi ya aina mbalimbali za nyavu za uvuvi baada ya kupata malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wavuvi ambao wamekuwa wakilalamikia baadhi ya nyavu ambazo wanatakiwa kuzitumia kisheria kwa ajili ya uvuvi kutokuwa na sifa ya kukamata mazao ya samaki katika maeneo yao.

Amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Dk. Rashid Tamatamah kuhakikisha kufikia Machi 23, mwaka huu awe amempatia taarifa hiyo ili iweze kutoa mwongozo wa maamuzi ya nyavu ambazo zina tija kwa shughuli za uvuvi.

Katika mkutano huo wa hadhara na wananchi wa Kata ya Jibondo Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani, Waziri Ndaki amepiga marufuku kitendo cha baadhi ya maafisa uvuvi kuwakamata wafanyabiashara wa samaki waliyopo mitaani yakiwemo maeneo ya kuuzia vyakula kwa madai samaki wanaouzwa katika eneo hilo hawana sifa kisheria badala yake watafute vyanzo vya maeneo ambayo watu wanavua samaki hao.

“Kuna mambo ambayo sipendi sitaki kabisa kusikia afisa uvuvi anaenda sokoni kutafuta samaki ambao wapo kinyume cha sheria na kuwanyanyasa akinamama wanaokaanga samaki, wakiona samaki wa namna hiyo wanapaswa kuwauliza aliyewauzia ili wapate chanzo halisi cha samaki walipovuliwa badala ya kumnyanyasa mfanyabiashara ambaye anauza chakula au kununua samaki anapeleka nyumbani kwa ajili ya mboga,” amefafanua Ndaki

Kuhusu kilimo cha zao la mwani Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Dk. Rashid Tamatamah, amesema zao hilo limekuwa likilalamikiwa kwa kuuzwa kwa bei ndogo hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakulima hao wasipate mafanikio na kuwataka wakulima wasiingie mikataba ya kuuza zao la mwani badala yake wauze kwa wafanyabiashara ambao wanakuwa na bei nzuri yenye tija kwao.   

Dk. Tamatamah amesema wizara itahakikisha inasimamia zao hilo kwa kuwa limekuwa mkombozi mkubwa kwa akinamama wengi katika Ukanda wa Pwani pamoja na kuwataka waliongezee thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo sabuni.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Juma Ali amepongeza namna Wizara ya Mifugo na Uvuvi inavyohakikisha inasimamia maeneo ya hifadhi ya bahari kupitia Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) huku akitaka kutatuliwa kwa baadhi ya changamoto ambazo zinaleta hali ya kitengo hicho kushindwa kushirikiana na wananchi.

Ali amefafanua kuwa baadhi ya watumishi wa kitengo hicho wamekuwa wakishindwa kufanya kazi kwa kufuata ueledi wa kazi yao na kuweka maslahi binafsi hali ambayo imekuwa ikizorotesha hali ya uhifadhi ukizingatia Wilaya ya Mafia bado ina maeneo mengi ambayo yana wingi wa samaki kwa ajili ya shughuli za uvuvi.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliofika katika mkutano huo wamemuelezea Waziri Ndaki changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo na kuelezea namna walivyo na imani kubwa na waziri huyo katika kutatua changamoto zao ili waweze kufanya shughuli za uvuvi bila bughudha na waweze kufuata sheria za nchi.

Aidha, Waziri Ndaki akiwa katika Kata ya Kilindoni Wilayani Mafia, amezungumza na baadhi ya wavuvi na kuwataka wafanye shughuli za uvuvi kwa kutumia taa nyakati za usiku wakati Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiendelea kufanya tafiti ya taa bora zaidi ambazo hazina madhara wakati wa kuvua samaki.

Aidha, amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kulalamikiwa na baadhi ya wavuvi kushindwa kufanya shughuli zao nyakati za usiku kwa kuzuiwa kutumia taa kama chambo kwa ajili ya kukamatia samaki.

Waziri Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani akiambatana na Naibu Waziri, Pauline Gekul, ambapo Waziri Ndaki amepata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wavuvi na kujionea hifadhi ya bahari na maeneo tengefu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles