LONDON, Uingereza
KWA kutumia gazeti la the Telegraph, Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson amesema kuna masuala ”zaidi tunapaswa kufanya” kupambana na ubaguzi wa rangi.
Kutokana na hali hiyo, Johnson ametangaza tume mpya kutazama ”aina zote za hali ya kutokuwepo kwa usawa.”
Johnson alisema ” hakuna mtu yeyote anayejali kuhusu nchi hii anayeweza kupuuza maandamano ya kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi yaliyojitokeza baada ya kifo cha George Floyd.
Lakini mbunge wa chama cha Labour, David Lammy alisema kuwa ni wakati wa kuchukua hatua sasa na si tathimini nyingine.
Alisema Uingereza isijaribu ”kuandika upya historia ya zamani” kwa kuondoa alama za kihistoria.
Urithi wa Uingereza uachwe ”kwa amani” aliongeza.
Johnson alikemea ”Magenge ya watu wa mrengo wa kuliza” waliohusika kwenye maandamano ya vurugu siku ya Jumamosi , yaliyosababisha zaidi ya watu 100 kukamatwa jijini London, baada ya maelfu kukusanyika wakisema wanazilinda sanamu.
Hatua hiyo ilikuja baada ya sanamu moja kwenye viwanja vya bunge kuandikwa maneno kwa rangi ” alikuwa mbaguzi” mwishoni mwa juma lililopita mjini Bristol, waandamanaji dhidi ya ubaguzi wa rangi waliangusha sanamu ya mfanyabiashara wa utumwa Edward Colston.
Maelfu ya watu wameandamana nchini Uingereza kama sehemu ya maandamano ya Black Lives Matter, baada ya kifo cha Floyd mjini Minneapolis mwezi uliopita.
Alisema anaunda tume kutazama hali ya kutokuwa na usawa kwa kuwa ”haina maana tu kusema kuwa tumefanikiwa kupambana na ubaguzi wa rangi”.
Aliandika: ”Kuna mengi ya kufanya na tutayafanya. Ni wakati kwa tume kutathimini suala ya usawa katika ajira, afya, elimu na maeneo mengine.”
Maswali kuhusu kutokuepo kwa usawa katika sekta ya afya, yamekuwa yakijitokeza wakati wa janga la virusi vya corona, baada ya takwimu kuonesha kuwa watu wa jamii ya wachache wamekua wakipoteza maisha zaidi kutokana na virusi vya corona.
Waziri kivuli wa Sheria, David Lammy alisema idadi kadhaa ya malalamiko kuhusu ubaguzi wa rangi yametolewa, kama vile ripoti yake mwenyewe kuhusu wanavyotendewa watu weusi, raia wa Asia na watu wa jamii ya walio wachache
”Unaweza kuelewa kwanini mara nyingine Uingereza tunataka takwimu, data, lakini hatutaki kuchukua hatua,” aliiambia BBC Radio 4.
”Watu weusi hawatafuti visingizio kama Boris anavyoashiria, wanaandamana hasa kwa sababu muda wa tathimini umekwisha na sasa ni muda wa kuchukua hatua.”
Waziri huyo kivuli ametoa wito kwa bunge na mapendekezo ya tathimini zilizofanyika awali kufanyiwa kazi.
Simon Woolley, mwanzilishi wa operesheni ya Black Vote na mwenyekiti wa chombo kinachotazama masuala ya usawa , amesema ” ametiwa moyo” na tangazo kuhusu kuundwa kwa tume.