NA MWANDISHI WETU
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, leo Julai 27, 2021, amepokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi wa tukio la moto uliotokea katika soko Kuu la Kariakoo Julai 10, 2021 jijini Dar es salaam.
Waziri Majaliwa amepokea ripoti hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati, CP Liberati Sabas na kuahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati.
Akizungumza baada ya kuipokea taarifa hiyo kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Majaliwa amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa tume hiyo kwa kazi nzuri iliyofanyika kwa weledi mkubwa.
Majaliwa amesema ataifikisha taarifa hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu, kwani tukio hilo limewagusa watu ndani na nje ya nchi.
“Naahidi mbele yako mwenyekiti kuwa Serikali imeridhishwa na taarifa mlioyo nikabidhi leo na mapendekezo yote mliyoyatoa yatazingatiwa,”amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo CP Sabas, amezishukuru Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wajumbe wengine katika timu hiyo kwa ushirikiano walioutoa katika kufanikisha kazi hiyo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu kama haya tuliyoyabaini yakifanyiwa kazi matukio kama hayo hayatajirudia,” amesema CP Sabas.
Julai 11, 2021, Waziri Majaliwa alipotembelea na kukagua hatua zinazoendela kuchukuliwa kudhibiti moto katika soko la kimataifa la Kariakoo alitangaza kamati ambayo ilipewa kazi ya kuchunguza tukio hilo ili kubaini chanzo cha moto huo.
Kamati hiyo aliyoundwa ilifanya kazi na Kamati ya Ulinzi na Usalama iliyoanza kufanya kazi chini ya Mkuu wa Mkoa huo ilijumuisha Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu (Idara ya Maafa).
Wengine ni Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikujumuisha Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Zimamoto, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU).
Pia Waziri Mkuu alizitaja Wakala wa Majengo, Shirika la Umeme (TANESCO), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Taifa ya mashtaka, Wakala wa Umeme na Ufundi Tanzania (TEMESA)