25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI MKUU AGUSA JIPU BUTIAMA

*Ambakiza naibu waziri kuchunguza  upotevu wa mamilioni

Na Shomari Binda,Musoma


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amegusa jipu la upotevu wa mamilioni ya fedha, huku akimwagiza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.

Alisema halmashauri hiyo, imekuwa na tabia ya kutumia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo zinazotolewa na Serikali katika shughuli nyingine jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ambapo aliagiza kuchunguzwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Solomon Ngiliule, Mweka Hazina wa Halmashauri, Masanja Sabuni na Ofisa Manunuzi wa Halmashauri  hiyo, Robert Makendo.

Alisema viongozi hao wanatakiwa wachunguzwe kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali zikiwamo Sh milioni 12 walizotumia kuandaa historia ya halmashauri hiyo.

Alisema fedha zingine, ni Sh milioni 70 za elimu maalumu, Sh milioni 288 za mradi wa maji Butiama ambazo zote hazijulikani zilivyotumika.

“Hatuwezi kuvumilia vitendo hivi fanyeni uchunguzi na naomba taarifa yake mara mtakapokamilisha,” alisema.

Ili kuhakikisha kazi ya uchunguzi inafanyika haraka, Majaliwa alimwagiza Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Josephat Kandege, kubaki  Butiama ili kuhakikisha ukaguzi huo maalumu unafanyika juu ya fedha zinazotumwa na Serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ya halmashauri hiyo.

 

“Zilitolewa  zaidi ya Sh milioni 200 kwenye akaunti ya maendeleo, badala ya kutumika kwenye miradi ya maendeleo zilitumika kulipa posho kwenye mitihani ya kidato cha nne.

“Mbaya zaidi zilitumika kulipa posho za madiwani 2014/15, ambao walikuwa madarakani kabla ya sisi kuingia madarakani.

“Pia Shilingi milioni 90, zilitumika kutengeneza historia ya wilaya…jamani hiki si kitu kidogo cha kuandika inakuaje zinatumika fedha nyingi ya kuandaa…naomba uchunguzi ufanyike haraka, ikibainika kuna shida hatua za haraka zichukuliwe kwa wote watakaohusika”, alisema Majaliwa.

Alisema  pia kuna matumizi  ya mamilioni ya fedha  kinyume cha taratibu bila kufuata maelekezo, huku akisema fedha nyingi badala ya kutekeleza miradi ya maendeleo zimetumika kulipana posho.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa  (Takukuru) mkoani Mara imkamate na kumuhoji Meneja wa Wakala wa Majengo  Tanzania (TBA) mkoani Mara, Mhandisi Peter Salim  baada ya kushindwa kutekeleza ujenzi wa mradi wa ofisi za halmashauri ya wilaya ya Butiama.

Alisema  Serikali ilitoa Sh milioni 600 Aprili, mwaka jana, kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi za halmashauri ya wilaya hiyo, lakini hadi sasa wakala huo haujafanya kazi yoyote.

Katika maelezo yake, Mhandisi Salim alisema ujenzi wa ofisi hiyo hadi kukamilika  utagharimu Sh bilioni tatu, kati ya Sh milioni 600 zilizotolewa na Serikali Sh milioni 400 zimetumika kujengea msingi, kauli ambayo ilipingwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Anna-Rose Nyamubi.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, si kweli kuna kazi inayoendelea bali kilichopo pale ni mashimo ambayo hayajulikani ni ya nini. Kuna jengo moja lilijengwa kwa mabati kama stoo na hakuna mafundi wanaoendelea na kazi”

Waziri Mkuu, alisema  Serikali iko katika mchakato wa kuboresha mazingira ya wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ofisi za watumishi na kwamba haitamvumilia mtu yeyote atayekwamisha juhudi hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles