24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

ACT WAZALENDO YAIPA TAHADHARI CCM

NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


CHAMA Cha ACT Wazalendo kimekitahadharisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuacha kufurahia wanachama wanaokimbilia ndani ya chama hicho kwani ipo siku watageuka na kurejea kwenye vyama vyao.

Akizungumza  na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa ACT (Bara), Msafiri Mtemelwa alisema kuhama wanachama katika vyama haikuanza leo hivyo ni vyema CCM ikajitafakari kwani ipo siku watalia.

“ Ninatoa tahadhari kwa CCM kuacha kufurahia wanachama wanavyokimbilia kwenye chama chao kwani mimi nawafananisha  wanaohama sawa na ndege aina ya tetele ambapo ipo siku watarejea kwenye pori walilolizoea,”alisema Mtemelwa.

Mtemelwa aliwatoa hofu wanachama wa ACT kuwa chama hicho kipo imara na kimejipanga vya kutosha hivyo hakitayumbishwa kamwe.

Alisema hawababaiki na kuondoka kwa baadhi ya wanachama hao ila wanachokiangalia kwa uzito kama wananchi wanakubali mageuzi.

“Kura zilizopatikana katika Uchaguzi Mkuu zaidi ya milioni sita kwa wapinzani zinaonesha dhahiri wananchi wanakubali mageuzi na wanataka mabadiliko,”alisema Mtemelwa.

Alisema hakuna asiyefahamu kwenye vyama vya upinzani kuna shida kubwa hivyo ni vyema wakaendelea kutiana moyo ili jahazi lifike salama.

Akizungumzia kuhusu ushiriki katika uchaguzi wa marudio kwenye majimbo ya Siha na Kinondoni, alisema chama hicho hakitashiriki uchaguzi kwa sababu uwanja wa demokrasia bado si sawa na kushiriki uchaguzi huo ni sawa na kuhalalisha mchakato haramu.

“ Sisi kama chama cha ACT msimamo wetu ni uleule bado hatutashiriki katika uchaguzi wa marudio kwenye majimbo ya Kinondoni na Siha pamoja na kata tisa uliopangwa kufanyika Februari 17, mwaka huu,”alisema Mtemelwa.

Alisema sababu kubwa ya kususa kwao ni kutokana na mambo yaliyolalamikiwa kwenye uchaguzi wa Januari 13, mwaka huu hazijabadilika  kwa sehemu kubwa.

“ Mageuzi madogo yaliyofanywa na tume ni kauli ya kuwataka wakuu wa wilaya kuacha kuingilia uchaguzi …hii ni tone dogo katika malalamiko ya vyama vya upinzani dhidi ya tume,”alisema Mtemelwa.

Alisema kamati ya uongozi  ya ACT ilikaa Novemba 8, mwaka jana na kuamua kusitisha ushiriki  katika uchaguzi  wa marudio na kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu kufanya tathimini juu ya ushiriki kwenye chaguzi hizo.

“ Kamati kuu iliamua rasmi kusitisha ushiriki wetu katika uchaguzi wa Januari 13, mwaka huu kwa sababu ya vitendo vya dola kuingilia uchaguzi na kulazimisha ushindi kwa CCM,”alisema Mtemelwa.

Alisema dosari zilizojitokeza katika uchaguzi uliopita ni pamoja na CCM na Serikali kuongeza matumizi ya mabavu kupitia vyombo vya dola na kuweka mazingira ya kushinda uchaguzi.

Pia chama kilihakikisha kinawatumia vyema watendaji wa halmashauri wanaohusika na usimamizi wa uchaguzi ambao wengi huteuliwa kwa misingi ya ukada wa CCM ili kushinda.

“ Mazingira yalipoonekana kuwaelemea , CCM ilitumia njia za kimabavu kama vile kuvamia pia kuteka viongozi na kisha kuwaweka mahabusu,”alisema Mtemelwa.

Alisema mbali ya kila mbinu kugonga mwamba CCM ilitumia vyombo vya dola kujitangazia ushindi kimabavu licha ya matokeo kuonekana wameshindwa.

Mtemelwa alisema NEC imeonekana kutojali hitilafu zilizojitokeza na kuchukua hatua za kurekebisha kabla ya kuitisha uchaguzi mpya.

Alisema ACT iliweka bayana mgomo wa uchaguzi wa Januari 13, mwaka huu kama hatua ya awali kushinikiza tume na vyombo vya dola kufanya mageuzi ya msingi kwenye mchakato wa uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles