Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama, amewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha wanaweka mkakati mzuri wa kusaidia kusambaza umeme vijijini kwa taasisi za serikali na dini.
Waziri Mhagama alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika kitongoji cha Shuleni, kijiji cha Chihurungi, iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, Julai 14,2024.
“Halmashauri yetu sasa imebakiza vijiji vinne tu, na hadi mwezi wa tisa mwaka huu, vijiji vyote vitakuwa vinawaka umeme, ikiwemo kijiji cha Nambendo kilichopo pembezoni ambapo tayari utandazaji wa nyaya za umeme unaendelea,” alisema Waziri Mhagama.
“Tuna shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu, na Waziri wa Nishati. Tunaendelea kuomba vitongoji vilivyoongezwa viwekwe umeme haraka,” aliongeza.
Wananchi wa Chihurungi wamehimizwa kutumia umeme huo vizuri ili kuleta faida fungamanishi za kiuchumi, ikiwemo viwanda vya chuma na viwanda vya kutengeneza magrili.
Awali, Wakala wa Nishati Vijijini na Msimamizi wa Mradi wa REA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Robert Ndule, alisema Chihurungi ni moja ya vijiji 28 vilivyokuwa vimebaki kupatiwa umeme katika Halmashauri ya Songea Vijijini.
“Kijiji hicho kina wigo wa wateja 64 na kwa sasa kimeunganisha wateja 9. Tunaendelea kutoa wito kwa taasisi za serikali na zisizo za serikali kutuma maombi ya kuunganishwa,” alisema Mhandisi Ndule.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea, Mtela Mwampamba, aligusia umuhimu wa wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya pamoja kwa familia, mfuko ambao unajumuisha watu sita kutibiwa kwa mwaka mzima.
“Ukiwa na bima ya afya, inasaidia kupata huduma za afya pindi magonjwa yanapojitokeza ghafla na ukiwa hauna fedha. Tutumie fursa hii tuliyonayo wakati wa mavuno kujiunga na bima ya afya,” alisema Mwampamba.