Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Waziri wa Afya, Jenister Mhagama amesema atahakikisha mchakato wa uanzishwaji Bima ya Afya kwa Wote unakamilika haraka kwa sababu magonjwa hayasubiri na hilo ndilo jukumu kubwa alilopewa.
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo Septemba 11,2024 baada ya kutembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Ubongo Muhimbili (Moi), ambapo changamoto kubwa iliyolalamikiwa na baadhi ya wagonjwa ni gharama kubwa za matibabu.
Baadhi ya wagonjwa wamesema wana maisha duni na kwamba wamelazimika kuuza mali zao kukidhi gharama za matibabu.
“Maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kokote aliko, tunaweza kuwa na tiba nzuri lakini zisipowafikia wananchi wanyonge hazitakuwa na faida.
“Kuna kazi kubwa iko mbele yetu hasa kwangu kuhakikisha bima ya afya kwa wote inafanikiwa na kwa sasa tunakamilisha uundwaji wa kanuni,” amesema Waziri Mhagama.
Amesema pia watakuwa wakali kuhakikisha matumizi ya fedha katika mfuko huo yanakuwa sahihi kuepuka udanganyifu unaoweza kuisababishia hasara Serikali.
Kuhusu taasisi hizo amezipongeza kwa ubunifu wanaoendelea kuufanya akisema anakusudia kuanzisha tuzo maalumu kushindanisha taasisi katika sekta ya afya kwenye kipengele cha utoaji huduma na bunifu za kibobezi.
Mkurugenzi wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, amesema wagonjwa wengi wanaridhika na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali wa rasilimali watu na vifaa.
“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa uwekezaji alioufanya katika sekta ta afya, watu wakipata huduma hapa wanafananisha kama zinazotolewa kule India, tutaendelea kuimarisha teknolojia ili tuweze kuwafikia wananchi sehemu mbalimbali kule walipo.
“Tiba utalii imezidi kuimarika katika kipindi cha miaka mitatu, kwa kila robo ya mwaka tunapata wagonjwa 343, inatuongezea fedha kwenye taasisi yetu ambazo zinakwenda kusaidia watu wasiokuwa na uwezo…nchi karibu 20 zinakuja,” amesema Dk. Kisenge.
Aidha amesema kupitia Samia Outreach Programme mpaka sasa wametembelea mikoa 16 ya Tanzania Bara na Zanzibar na kuona wananchi zaidi ya 17,000 ambapo wengine walikutwa na matatizo ya moyo na kutibiwa na wengine kufikishwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Amesema kwa siku wanafanya operesheni nne hadi tano na kuona wagonjwa 500.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Moi, Dk. Lemeri Mchome, amesema uwekezaji wa zaidi ya Sh bilioni 26 uliofanywa na Serikali katika taasisi hiyo umewezesha kutoa matibabu ya kibingwa na bobezi.
Amesema zaidi ya asilimia 96 ya magonjwa yote ya mifupa na asilimia 98 ya magonjwa ya mfumo wa ubongo na mishipa ya fahamu yanatibiwa hapa nchini kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali.
“Tunashukuru juhudi za mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji ambao ameufanya kwenye taasisi yetu wa vifaa tiba na rasilimali watu. Tutahakikisha kwamba tunaondoa kero zote na huduma zinapatikana kwa wananchi kwa wakati na ufanisi wa hali ya juu,” amesema Dk. Mchome.