*Katibu Mkuu Mahimbali Asema Vision 2030 Imelenga Kuvuta Uwekezaji Mkubwa, Kati
*Chemba ya Migodi Yawasisitiza Wadau Kuitendea Haki Tanzania
*Vijana Vyuo Vikuu Waomba Kukumbukwa
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ametoa wito kwa Kampuni, Taasisi na Watu binafsi wanaotarajia kushiriki Mkutano wa Mining Indaba kuhakikisha wanaiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa kutangaza utajiri wa madini na fursa za kiuwekezaji zilizopo.
Amesema kutokana na fursa mbalimbali katika Sekta ya Madini kuanzia kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji, utoaji huduma migodini na uongezaji thamani madini ni alama tosha ya kuitambulisha Tanzania kwa sauti moja kwa wadau mbalimbali watakaoshiriki katika mkutano huo mkubwa.
Waziri Mavunde ameyasema hayo wakati akifungua kikao maalum cha wadau wanaotarajia kushiriki katika mkutano wa Mining Indaba utakaofanyika kuanzia Februari 5 hadi 8, 2024 nchini Afrika Kusini.
Ameongeza kwamba, bado Sekta ya Madini nchini haijatoa mchango unaostahili kiuchumi ikilinganishwa na utajiri wa rasilimali madini pamoja na fursa zilizopo na kusisitiza kuhusu shughuli za utoaji huduma na usambazaji wa bidhaa migodini kuwa ni eneo ambalo kama Wizara inalichukua kwa uzito kutokana na manufaa yake na kwamba ni miongoni mwa maeneo ambayo imeyapa kipaumbele katika mkutano huo.
“Kuna baadhi ya nchi duniani wamejikita eneo moja tu la usambazaji wa bidhaa na utoaji huduma migodini. Tunataka watanzania wengi wanufaike kupitia eneo hili na tunapenda kuona uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazohitajika migodini zizalishwe zinafanyika hapa nchini,” amesisitiza Waziri Mavunde.
Akizungumzia suala la utafiti, Waziri Mavunde amesema ni eneo ambalo Tanzania inatarajia kulitangaza kupitia mkutano huo lengo likiwa ni kuvutia uwekezaji katika shughuli za utafiti wa madini na hususan madini mkakati ambayo ndiyo mwelekeo wa dunia kwa sasa kutumia madini muhimu na mkakati kuzalishaji nishati safi.
“Utafiti wakina utaiwezesha nchi yetu kupata kanzi data ya madini yetu, hatutaki iwe nchi ya kubahatisha, hatutaki wizara yetu kuwa inayoshughulikia migogoro kati ya wachimbaji wadogo na wawekezaji, tunataka wawekezaji wafurahie uwekezaji waona wachimbaji wachimbe bila kubahatisha na wakue,’’ amesema Waziri Mavunde.
Naye, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Philbert Rweyemamu akizungumza katika kikao hicho amewataka wote watakaoshiriki kuitendea haki Tanzania kwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mkutano huoili kutoka na matokeo chanya.
Aidha, Mhandisi Rweyemamu ameainisha shughuli mbalimbali ambazo Tanzania inatarajia kushiriki wakatiwamkutano huoni kutaja baadhi kuwa ni pamoja na kushiriki kikao cha Mawaziri wa Madini wa Afrika (Ministerial Symposium) na kuwa na siku maalum ya kuinadi Tanzania katika mkutano adhimu wa Mining Indaba.
Kwa upande wake, akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema kikao hicho ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ya kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini ambapo mkutano wa Mining Indaba ni moja ya mikutano ambayo wizara inategemea kuitumia kuendelea kuvutia uwekezaji.
Ameongeza kuwa, Tanzania inatarajia kuvutia wawekezaji wapya ili kuanzisha migodi ya kati na mikubwa ikiwemo kuongeza imani kwa wawekezaji waliopo nchini na wanaotarajia kuwekeza kwenye Sekta ya Madini
Mkutano wa Indaba ni moja ya mikutano mikubwa ambayo huwakutanisha wawekezaji wapatao 900, taasisi za kisekta 40 na watendaji wakuu wa kampuni kubwa wapatao 1000.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo umefadhiliwa na kampuni za Barrick Gold, Anglo Gold Ashanti, Tembo Nickel, Shanta Gold, Mantra Tanzania, TRX Gold, Petra Diamond, Orica, City Engineering na AUMS. Aidha, kikao cha wadau kimefadhiliwa na Benki ya Stanbic.