Mwandishi Wetu- Morogoro
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amefanya operesheni kubwa ya kukagua na kupima ulevi wa pombe kwa madereva wa mabasi na malori mjini Morogoro jana.
Lugola pia alizungumza na abiria wa mabasi hayo pamoja na viongozi wa madereva waliopo Kituo Kikuu Cha Mabasi Msamvu ambao walimwelezea kero mbalimbali zinazowakabili.
Ukaguzi wa mabasi na malori ulifanyika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro-Dar es Salaam ambako waziri huyo akiwa na kamanda wa polisi mkoa, mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa (RTO), alisimamisha vyombo hivyo vya moto vilivyokuwa vinaingia Mizani iliyopo Kihonda, nje kidogo ya Mji wa Morogoro.
Akizungumza na madereva, makondakta na wapiga debe alisema ni wajibu wake kufanya hivyo katika hatua ya kupunguza kwa kasi ajali mbalimbali zinatokana na uzembe wa madereva nchini.
Alisema ajali zimepungua hasa Mkoa wa Morogoro, kwa sababu ya askari wa usalama barabarani wamefanya kazi zao kiweledi na madereva wanafuata sheria.
Aliwaasa madereva kuacha uendeshaji wa mashindano, kuwa na leseni na pia kuhakikisha wanapokuwa barabarani wanakua makini.
“Madereva wa mabasi na malori ambao nimefanikiwa kuwapima ulevi wasiopungua sita, sijawakuta na ulevi, wapo makini na hii inaleta nguvu na imani kuwa madereva wanaelewa na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
“… na pia ndani ya mabasi niliyokuwa nayakagua nimezungumza na abiria wakaniambia madereva wanaendesha vizuri,” alisema Lugola.
Wakizungumza kwa wakati tofauti katika Kituo Kikuu cha Mabasi, madereva walilipongeza jeshi la polisi mkoani hapa kwa usimamizi mzuri ambao umewaunganisha na kuwafanya waifurahie kazi wanayoifanya.
Dereva Juma Rashidi wa basi linalosafiri kutoka Ifakara hadi Morogoro, alisema wanajisikia furaha kubwa kwa uongozi mpya mkoani humo.