28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Kanyasu aagiza TAWA waunde ‘Takukuru yao’

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KUTOKANA na tuhuma za rushwa kuwakabili baadhi ya  maofisa wanyamapori, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania( TAWA) kuunda chombo cha ndani cha kuzuia na kupambana na rushwa.

Akizungumza na maofisa wanyamapori hao jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Waziri Kanyasu alisema chombo hicho kitakuwa na wajibu wa kuchunguza mienendo ya rushwa kwa watumishi hao ikiwa pamoja na kuwakamata wale wote watakaojihusisha kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wananchi.

Mbali na jukumu hilo,chombo hicho kitashughulikia masuala ya nidhamu pamoja matumizi mabaya ya madaraka kwa watumishi.

Alisema chombo hicho kitakuwa na jukumu la kuchunguza vitendo vya rushwa kwa maafisa hao kabla ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutekeleza jukumu hilo ikiwa lengo ni kutaka kumaliza kabisa tatizo hilo.

” Ninataka  kabla ya TAKUKURU kuingia kwa ajili ya kuchunguza vitendo vya rushwa, chombo hiki kitakuwa tayari kimewabaini watumishi ambao wapo kwa ajili ya maslahi ya matumbo yao.Alisema Kanyasu

Akizungumzia namna  chombo hicho kitakavyofanya kazi, alisema chombo hicho kitafanya kazi nchi nzima na kitakuwa kila kanda na kusisitiza kuwa  hakitakuwa makao makuu pekee kama vilivyo vitengo vingine.

“Undeni hiki chombo haraka iwezekanavyo haiwezekani wote mnaonekana ni wala rushwa ilhali kuna watumishi wachache wanaoipaka matope Taasisi hii” alisisitiza.

Katika hatua nyingine,aliiagiza mamlaka hiyo ibadilishe fomu ambapo mifugo  ikikamatwa ndani ya hifadhi, mchungaji  atatakiwa kujaza baadhi ya taarifa muhimu ikiwemo kukiri mifugo kukutwa ndani Hifadhi.

Alisema hatua hiyo, inakuja baada ya kugundua  mapungufu makubwa kwenye fomu wanazozitumia kwa sasa, Kanyasu alisema fomu hizo mpya ziongezewe kipengele cha  muda ambao mifugo  imekamatwa na wakati huo, askari wanyamapori wanatakiwa kuipiga picha mifugo ikiwa vielelezo vya ushahidi vitakavyotumika mahakamani wakati wa kesi.

Naye, Naibu Kamishina wa TAWA, Mabula Misungwi amesema malalamiko mengi ya wananchi kuhusiana na wahifadhi yanahusu rushwa, kuundwa kwa chombo hicho kitasaidia kupunguza tatizo la rushwa kwa kuwabaini wale wote wenye tabia hizo.

Alisema chombo hicho kitasaidia kupunguza tatizo la kuwaona watumishi wote ni wala rushwa, jambo linalopunguza ari ya kazi kwa baadhi ya watumishi wanaofanya kazi kwa misingi ya kufuata kanuni na sheria za utumishi wa Umma

Naye Ofisa Wanyamapori, Abel Kazoka alisema kuundwa kwa chombo hicho kutasaidia kuwabaini wala rushwa, badala ya kuwaona watumishi wote wa taasisi hiyo ni wala rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles