27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Waziri Kakunda isafishe Brela haraka

KATIKA toleo la jana la gazeti hili tulichapisha habari kuhusu kauli ya Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda akieleza kusikitishwa kwake na madudu yanayofanyika katika ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).

Alisema kuna madudu mengi ambayo hayapaswi kufumbiwa macho katika ofisi hizo kutokana na kuwapo na utitiri mkubwa wa matapeli (vishoka) ambao kwa namna moja au nyingine wanashirikiana na wafanyakazi wa Serikali.

Tena kibaya zaidi, Waziri Kakunda hakuficha hisia zake na kuamua kusema hadharani kuwa vishoka hao wamefikia hatua mbaya hadi kumtapeli aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba. Tunasema hali hii inatisha.

Kutokana na uozo huu, Waziri Kakunda alilazimika kutoa siku 14 kwa wakala huo kujitathmini na kujisafisha haraka kabla ya kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wahusika.

Hali inavyoelekea ndani ya wakala huu si shwari, kwa sababu kitendo cha waziri mwenye dhamana kufanya ziara mara mbili ndani ya wiki mbili si jambo dogo. Kuna tatizo kubwa.

Hali hiii nadhihirishwa na kujaa kwa malalamiko mengi ya utoaji huduma ambayo yanaonesha wazi kuna mtandao mkubwa wa vishoka wanaoshirikiana na watumishi wa Serikalikuwapata waombaji vibali ili kujipatia fedha za haramu.

Tabia kama hii ilishamiri maeneo makubwa kama vile ndani ya Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini kazi kubwa ilifanyika huko ya kuondoa vishoka na sasa hali imetulia.

Waziri Kakunda, tunakushauri usisubiri muda uliotoa ndo uchukue hatua, anza sasa maana inaonekana wazi hali ndani ya wakala huu ni mbaya. Inahitaji hatua za harakamno kuweka mambo sawa. Tunasema isafishe Brela haraka.

Kusubiri mudahuo wakati kuna Watanzania wengi wanaendelea kutapeliwa  mamilioni ya fedha na vishoka hawa ambao wamejenga mtandao mkubwa wa wafanyakazi wa wakala huu si jambo lenye afya.

Eneo la chini la jengo lenye ofisi za wakala huu ndiyo sehemu ambayo imegeuzwa kuwa machinjio ya watu wema wanao kwenda kusajili nyaraka mbalimbali ambazo wanazihitaji, ambako hukumbana na vishoka wenye ‘viofisi vyao’ eneo hili, kwa madai eti wana wasaidia wananchi ambao hutoa hadi Sh milioni tatu.

Kwa kuwa eneo hili linaonekana wazi ni jipu ambalo limeiva, hapana shaka linapaswa kutumbuliwa.

Waziri Kakunda umefika wakati usisubiri upewe maelekezo na rais ndo uchukue hatua.

Malalamiko mengi ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi ndani ya wakala huu, ni kukaguliwa kwa mitambo iliyofungwa ambayo inadaiwa haifanyi kazi sawa sawa, lakini tovuti nayo imekuwa na mkanganyiko wa mambo mengi ambayo yanapaswa kuondolewa.

Sisi MTANZANIA, tunamshauri Mtendaji Mkuu wa Brela, Emmanuel Kakwezi  kuonesha kuwa yupo na aanze kuchukua hatua kwa sababu chombo anachokiongoza kimebeba dhamana kubwa ya uchumi wa taifahili.

Tunamaini kwa pamoja kati ya Kakwezi  na wasaidizi wake, watazingatia na kusimamia maagizo ya waziri ili kuhakikisha taswira yawakala huu haiendelei kuchafuliwa na kundi la watu wachache.

Tunamalizia kwa kumshauri Waziri Kakunda kuwa Brela isafishwe haraka iwezekanavyo kabla ya mambo kuharibika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles