Na Walter Mguluchuma-Katavi
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inatarajia kutoa ajira kwa watumishi wa kada mbalimbali za afya.
Imesema watakaopewa kipaumbele ni wale wakataoomba kufanya kazi mikoa ya pembezoni ambayo ina upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati alipokuwa akihutubia wakazi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi na kufungua upimaji na utoaji tiba wa magonjwa yasiyoambukiza.
Alisema Serikali inatarajia kutangaza ajira za watumishi 52,000 wa kada mbalimbali hivi karibuni, hivyo kwa nafasi za ajira zitakazotolewa zitagusa mikoa tisa.
Alisema watakaoomba kupangiwa kufanya kazi Mkoa wa Dares Salaam hawatakuwa na nafasi ya kuchaguliwa kwanza, kwani mkoa huo hauna tatizo kubwa.
Aliitaja mikoa yenye uhaba wa wataalamu kuwa ni Katavi, Rukwa, Kigoma, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Geita na Kagera.
Alisema tayari wizara yake imeandaa muswada kwa ajili ya kuupeleka bungeni ili ujadiliwe na hatimaye uwe sheria itakayowezesha kila mtu ajiunge na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu Raphael Muhuga, alisema Katavi ina watumishi 692 kati ya 2,174 wanaohitajika.
Alisema kuna upungufu wa watumishi 1,186 sawa na asilimia 69 ya mahitaji.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Katavi, Anna Shumbi, alisema mkoa huo unaongoza kwa mimba za utotoni.