25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri ahofia uagizwaji dawa za binadamu kwa magendo

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

SIKU chache baada Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kubainika kuwapo sokoni dawa bandia za binadamu za vidonge vya Duo-cotexcin, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameleza  wasiwasi wa kuwapo njia za magendo za kuagiza dawa nje.

Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya makabidhiano ya msaada wa dawa na vifaa tiba vilivyotolewa na   India.

“Mifumo yetu ipo imara na ndiyo maana TFDA imeweza kubaini dawa bandia sokoni, changamoto kubwa ambayo tunaiona ni uingizwaji wa dawa kwa njia za panya.

“Tunashukuru mtengenezaji wa dawa halali wa China ndiye aliyebaini na kuijulisha TFDA (kuwapo   dawa bandia) ikafanya uchunguzi na kuzikamata zile bandia.

“Bado haijabainika zimetoka nchi gani, huenda wahusika wapo nchini, wanatumia ujanja.

“Lakini wajue wazi kwamba tupo makini, naipongeza TFDA  kwa kazi nzuri ya ukaguzi na udhibiti wa ubora wanaoufanya.

“Wazalishaji na waingizaji wa dawa nchini wasidhani wakishaleta dawa sisi tumefunga mikono, tunafanya ‘post market surveillance’.

“Watu wetu wataibuka, wataingia kwenye maduka mitaani na kuangalia kama dawa ni salama au si salama.

“Nawataka TFDA wasiangalie ubora wa dawa punde inapoingia tu, waendelee kwenda katika maduka ya dawa, wachukue dawa waendelee kuipima kuangalia kama ina ubora unaotakiwa ama laa,” alisema.

Waziri Ummy aliwasihi wananchi kuendelea kununua dawa katika maduka yaliyosajiliwa na si yale ambayo hayajasalijiwa.

“Yapo ambayo hayajasajiliwa, ndiyo maana nina ‘ka-ugomvi’ fulani na maduka ya dawa ya mijini, sisi tunasema sasa hivi dawa si kama bidhaa nyingine, mfano kiatu au nguo.

“Dawa ni bidhaa ‘very sensitive’ inaweza kuua ndiyo maana tunataka ziuzwe kwenye duka la dawa ambalo kuna mfamasia.

“Wapo watu zamani walikuwa wana maduka ya dawa baridi mijini, wakati tukitambua kuna changamoto tunataka haya maduka yawepo nje ya miji.

“Wao wanasema hapana wanataka wakae mijini lakini lengo letu lazima tusimamie ubora wa dawa,” alisema.

Awali akipokea msaada wa dawa za India, alisema zina thamani ya   Sh. bilioni mbili na kwamba vitagawanywa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya vya serikali.

Waziri  alisema kwa sasa hali ya upatikanaji dawa muhimu nchini imeimarika kwa sababu  kiwango kimeongezeka kutoka asilimia 34 hadi  zaidi ya asilimia 85.

Balozi wa India nchini, Sandeep Arya, alisema hatua hiyo ni makubaliano kati ya Rais John Magufuli na Waziri Mkuu wa nchi hiyo,  Narendra Modi, alipofanya ziara nchini Julai 9 hadi 10, 2016.

“Madawa haya yanajumuisha yale ya kukabiliana na maambukizi mbalimbali, chanjo, upasuaji na matibabu mengine,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles